Kupewa utawala Umar ibn Khatab

Kupewa utawala Umar ibn Khatab

Abubakr anampa ukhalifa jamaa yake Umar, na anakhalifu maandiko yaliyo wazi kuhusu jambo hilo.Amesema Imam Ali (a.s) kuhusiana na suala la Ukhalifa: "Ama Wallahi ameuvaa (Ukhalifa) mtoto wa Abu Quhafa hali ya kuwa anajua kabisa kwamba nafasi yangu katika huo Ukhalifa ni kama nafasi ya mpini ulioko kwenye jiwe la kusagia nafaka." Akielezea kwa njia ya kinaya Imamu (a.s.) anasema:

"Hububujika kutoka kwangu fadhila kwa vile Mungu alinienzi kwa kuniweka karibu na materemkio ya wahyi, hivyo basi nilijizuia nikakaa mbali nao, nikawa nafikiri kati ya kuingia vitani hali nikiwa mikono mitupu, au nivute subira katika giza lililoshona hakika mtu mzima huzeeka, na mtoto huwa kijana. Muumini atataabika kwa juhudi kubwa kubakia na imani safi katika hali hiyo mpaka akutane na Mola wake."

Anaendelea kusema, "Niliona kusubiri ni bora na ni hekima, basi nikasubiri hali katika macho kuna tongo tongo na shingoni kuna mwiba umenasa, naouna urithi wangu nimenyang'anywa. Wa kwanza akaenda kisha akampasia mtoto wa Khatab baada yake, ajabu ilioje kwamba yeye (Abubakr) alitaka kujitoa katika ukhalifa alipokuwa hai na ampasie mwenzake ashike baada ya kifo chake ili kudhibiti walichokigawa nusu mbili, kila mmoja akawa mgumu hagusiki na anajikwaakwaa akitaka udhuru."

Kila mwenye kuhakiki na kutafiti atafahamu kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliutangaza ukhalifa na kumbainisha Ali ibn Abi Talib kabla ya kufa kwake kama ambavyo. wengi wa Masahaba wanalifahamu hilo na wakitanguliwa na Abubakr na Umar.

Na ndiyo maana Imam Ali alikuwa akisema. "Hakika yeye anajua kabisa kwamba, nafasi yangu katika huo ukhalifa ni kama nafasi ya mpini ulioko kwenye jiwe la kusagia." Na huenda hilo ndilo lililowafanya Abubakr na Umar wazuwie kusimuliwa hadithi za Mtume (s.a.w.w.) kama tulivyotangulia kueleza katika mlango uliopita, na wakashikamana na Qur'an kwa kuwa Qur'an japokuwa ndani yake (imo) aya ya Wilayah lakini jina la Ali halikutajwa wazi wazi kama ilivyo ndani ya hadithi za Mtume kwa mfano Mtume (s.a.w.w.) aliposema "'Yeyote ambaye mimi nilikuwa mtawala wake, basi huyu Ali ni mtawala wake." Na alisema Mtume: "Ali anatokana nami, nami natokana naye, naye ni mtawala wa kila muumini baada yangu."

Na kwa ajili hiyo tunafahamu kiwango cha mafanikio ya sera aliyoiandaa Abubakr na Umar katika kuzuwia na kuchoma moto hadithi za Mtume (s.a.w.w.), na wakaweka vizibo juu ya vinywa ili Masahaba wasizizungumze hadithi hizo kama tulivyotangulia kueleza ndani ya riwaya ya Qurdhah ibn Ka'ab. Vizuizi hivyo viliendelea kwa robo karne ambao ni muda wa utawala wa Makhalifa watatu hadi pale alipokuja Imam Ali kwenye Ukhalifah akawashuhudisha Masahaba ile hadithi ya Ghadir.

Masahaba thelathini walishuhudia, kumi na saba miongoni mwao ni katika wale waliopigana vita ya Badri. Hii dalili wazi inayoonesha kwamba, Masahaba hawa thelathini wasingeweza kuzungumza hivyo lau kama Amirul-Muuminina Ali (a.s) asingewataka kufanya hivyo, na lau Ali asingekuwa Khalifa na ameshika nguvu za utawala, basi woga ungewafanya wakakaa chini kimya wasishuhudie hilo kama yalivyotokea hayo kwa vitendo kutoka miongoni mwa baadhi ya Masahaba ambao hofu na husuda iliwakalisha chini wasishuhudie. Mfano wa hao ni Anas ibn Malik, Bar-raa ibn Azib, Zaid ibn Ar-qam na Jarir ibn Abdillah Al-bajali. Kwa tendo lao hilo la kunyamaza waliwapatwa na madhara makubwa kutokana na dua ya Imam Ali ibn Abi Talib (a.s).

Na wala Abu Turab (Imam Ali a.s.) hakuneemeka na Ukhalifa huo kwani siku zake zote zilikuwa ni mitihani, fitina, njama na vita dhidi yake vilivyoelekezwa kwake kutoka kila pande. Zilijitokeza zile chuki na mafundo ya zama za Badri, Hunain na Khaibar, mpaka alipouawa kishahidi nahizo Sunna za Mtume hazikupata sikio lenye kuzisikiliza mbele ya hao waliotengua na kuvunja viapo vyao, bali walitoka katika dini na ni waongo (waliotumia dini kwa maslahi yao) ambao walikwisha zowea kutenda maovu, rushwa na kuipenda dunia katika zama za Ukhalifa wa Uthman. Kwa ajili hiyo mwana wa Abu Talib hakuweza kurekebisha maovu yaliyotendwa kwa robo karne katika muda wa miaka mitatu na minne ila kwa kuiangamiza nafsi yake, na haiwezekani yeye kuiangamiza nafsi yake kwani yeye anasema:

"Wallahi mimi nafahamu mno ni kitu gani kitakachowafanyeni muwe wema, lakini siwezi kukurekebisheni kwa kuiangamiza nafsi yangu." Na haukupita muda mrefu isipokuwa Muawiyah ibn Abi Sufiyan aliukalia ukhalifa, akaziendeleza sera zile kama tulivyotangulia kusema, akazuwia hadithi isipokuwa zile zilizokuwepo zama za Umar. Yeye alikwenda mbele zaidi kuliko hivyo, akateua kikundi miongoni mwa Masahaba na Tabiina ili waweke hadithi (za uzushi) na hapo ndipo Sunna ya Mtume (s.a.w.w.) ikapotea ndani ya bahari hiyo kubwa ya hadithi za uzushi ziliundwa, na ngano zinazohusu fadhila za Masahaba.

Baada ya hapo Waislamu wakaendelea hivyo kwa karne nzima wakiwa ndani ya sunna za Muawiyah na zikawa ndizo zinazofuatwa na Waislamu wote. Tunaposema sunna za Muawiyah, maana yake ni sunna aliyoiridhia Muawiyah miongoni mwa matendo ya Makhalifa watatu, Abubakr, Umar na Uthman na yale aliyoyaongeza yeye na wafuasi wake miongoni mwa uzushi na uongo, ikwemo kumlaani na kumtukana Imam Ali na watu wa nyumba yake na wafuasi wake miongoni mwa Masahaba wema.

Kwa sababu hiyo basi, ninarudia kukariri kwamba,"Abubakr na Omar walifanikiwa katika sera hii ya kufuta sunna ya Mtume (s.a.w) kwa madai ya kuirejea Qur'an." Bila shaka utaona leo hii baada ya kupita karne kumi na nne, pale utakapotoa hoja kwa sunna madhubuti ya Mtume kuthibitisha kwamba, Mtume (s.a.w.w.) alimbainisha Ali kuwa ndiyo khalifa wake, hapo hapo utaambiwa, "Achana na sunna ya Mtume ambayo ndani yake kunahitilafu nyingi, kinatutosha kitabu cha Mwenyezi Mungu na kitabu cha Mwenyezi Mungu hakikutaja kwamba Ali ndiyo khalifa wa Mtume bali kimesema kuwa, mambo ya Waislamu yanakwenda kwa kushauriana."

Na hii ndiyo hoja yao, kwani sijazungumza na yeyote miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni isipokuwa, Shuraa ndicho kitambulisho chao na ndiyo mila yao. Pamoja na kwamba ukhalifa wa Abubakr ulitimia bila kutegemewa, na eti Mwenyezi Mungu aliwakinga Waislamu kutokana na shari, lakini cha ajabu ni kwamba haukupatikana kwa kushauriana kama wanavyodai baadhi yao, bali ulipatikana kwa ghafla na tena kwa nguvu, shinikizo na vitisho, na wengi miongoni mwa Masahaba bora waliupinga wakiongozwa na Imam Ali ibn Abi Talib, Sa'ad ibn Ubbadah, Ammar ibn Yasir, Salman, Miqadad, Zubair, Abbas na wasiokuwa hawa kama walivyoeleza wanahistoria wengi waliozungumzia tukio hili.

Hebu tulipuuze tukio hili na tuone Abubakr alivyomtawaza Umar baada yake na tuwaulize Masunni ambao wanategemea msingi wa mashauriano.

Swali:
Je, ni kwa nini Abubakr alimbainisha Umar kuwa khalifa wake na akawalazimisha Waislamu wakubali bila ya kuwaachia washauriane kati yao kama mnavyodai (shuura)? Ili ikubainikie zaidi, na kama ilivyo kawaida yetu kwamba hatutoi ushahidi isipokuwa kwa kutumia vitabu vya Masunni, sasa namletea msomaji namna Abubakr alivyomtawalisha jamaa yake.

Ibn Qutaibah ameandika ndani ya kitabu chake; Tarikhul-khulafai katika mlango unaohusu maradhi ya Abubakr na kumtawaza kwake Umar (r.a.) amesema: ...Kisha akamuita Uthman ibn Affan akamwambia: "Andika usia wangu." Akamtamki na Uthman akaandika; "Bismillahir-Rahmanir-Rahiim, huu ndiyo usia aliousia Abubakr ibn Abi Quhafah mwishoni mwa uhai wake duniani hali yakuwa anaondoka, na ni mwanzoni mwa uhai wake wa akhera akiwa ndiyo anaingia ndani yake. Hakika mimi nimemtawalisha juu yenu Umar ibn Khatab, iwapo mtamuona kuwa ni muadilifu miongoni mwenu basi hiyo ndiyo dhana yangu kwake na ndiyo matarajio yangu ndani yake, na iwapo atabadili na kugeuza mimi nilichokikusudia ni kheri na sijui ghaibu na hivi karibuni watajuwa wale waliodhulumu ni mgeuko gani watakaogeuka." Kisha akaufunga waraka huo na akampa.

Muhajirina na Ansari wakaingia kwake waliposikia kwamba yeye Abubakr amemtawalisha Umar wakasema: "Tunakuona umemtawalisha Umar juu yetu na bila shaka wewe unamfahamu na unaujua ukali wake kwetu sisi hali yakuwa wewe uko nasi basi itakuwaje utakapotoweka nawe utakutana na Mwenyezi Mungu na atakuuliza, sasa utasemaje?" Abubakr akasema:

"Ikiwa Mola wangu ataniuliza bila shaka. nitasema kuwa, nimemtawalisha juu yao mtu ambaye ni mbora wao katika nafsi yangu. Kuna baadhi ya wanahistoria kama vile Tabari na Ibnul-athir wanaeleza kwamba, Abubakr alipomuita Uthman ili aandike usia wake, alizimia wakati akimtamkia, basi Uthman akaliandika jina la Umar ibn Khatab.

Alipozindukana akasema soma uliyoyaandika, akasoma na akataja jina la Umar, basi Abubakr akasema: "llikuwaje ukafanya hivi?" Uthmani akasema, "Hukuwa ni mwenye kumvuka Umar." Abubakr akasema, "Umepatia." Alipomaliza kuandika watu fulani miongoni mwa Masahaba waliingia kwa Abubakr, akiwemo Tal-ha na akamwambia Abubakr, "Utasema nini kwa Mola wako kesho nawe umekwisha mtawalisha juu yetu mtu mkali na msusuavu, nafsi za watu zitatawanyika na nyoyo zitamkimbia."

Abubakr akasema:
"Niegemesheni." alikuwa kalala, wakamuegemesha, akamwambia Tal-ha, "Hivi unanikhofisha Mwenyezi Mungu atakaponiuliza jambo hilo kesho? Nitamwambia kuwa, nilimtawalisha juu yao mbora wa watu wako. . Na ikiwa wanahistoria wanaafikiana juu ya Abubakr kumtawalisha Umar bila ya kuwashauri Masahaba, basi tunaweza kabisa kusema kwamba, "Yeye alimtawalisha Umar bila ridhaa ya Masahaba na hali ya kuwa wamekasirika."

Na ni sawa sawa Ibn Qutaibah aliposema kuwa, Muhajirina na Ansari waliingia kwa Abubakar wakambwambia: "Bila shaka wewe unafahamu ukali wake kwetu sisi." Au kama alivyosema Tabari kwamba, "Waliingia kwa Abubakar watu fulani miongoni mwa Masahaba akiwemo Tal-ha na akamwambia Abubakr,

"Utasema nini kwa Mola wako kesho wakati wewe umemtawalisha juu yetu mtu mkali na msusuavu, nafsi za watu zitatawanyika na nyoyo zitamkimbia." Basi matokeo yake ni ya aina moja nayo ni kwamba mambo ya Masahaba hayakuwa ya mashauriano na hawakuwa wameridhia kutawalishwa Umar, jambo hilo alililazimisha Abubakr bila ya kuwashauri. Kilichotokeo kile kile ambacho Imam Ali (a.s.) alikizungumza wakati alipolazimishwa na Umar ibn Khatab kumbai Abubakr ambapo Imam Ali alisema, "Mnufaishe leo hii naye kesho atakurudishia."

Hali hii moja kwa moja ndiyo ile aliyoisema mmoja wa Masahaba kumwambia Umar ibn Khatab pale alipotoka na ile barua ambayo ndani yake umo usia wa ukhalifa, yule Sahaba akamwambia, "Ewe Baba Hafsi kuna nini humo ndani ya barua hiyo?" Umar akasema: "Sifahamu, lakini mimi nitakuwa wa kwanza kusikiliza na kuitii." Basi yule mtu akasema: "Lakini mimi Wallahi najua kilichomo, wewe ulimtawalisha kipindi kilichopita basi na yeye amekutawalisha mwaka huu."

Hii inatubainikia wazi kwamba, hapana shaka ndani yake kuwa, ule msingi wa Shuraa (mashauriano) ambao Masunni wanaupigia ngoma, hauna maana kwa Abubakr na Umar au kwa maelezo mengine ni kwamba Abubakr ndiyo wa kwanza kuubomoa msingi huu na kuupuuza na kufungua mlango kwa watawala wa Kibanu Umayyah waurudishe kuwa ni Ufalme wa Kaisari.

Watoto wanarithiana na baba zao, na vile vile ndiyo walivyofanya Banu Abbas baada ya Banu Umayyah, na hiyo nadharia ya Shuraa ikabaki kuwa ni ndoto inayowadanganya Masunni, haikuthibitika hapo zamani na wala haitathibitika. Jambo hili linanikumbusha mazungumzo yaliyofanyika kati yangu na mwanachuoni fulani miongoni mwa wanachuoni wa Kiwahabi kutoka Saudia ndani ya Msikiti mmoja mjini Nairobi Kenya. Mazungumzo yetu yalihusu utata wa ukhalifa, nami nilikuwa nikitetea maandiko yanayohusu ukhalifa na kwamba jukumu lote (la kuteua khalifa) ni la Mwenyezi Mungu na huliweka mahala atakapo na watu hawana hiyari na hawawezi kuliingilia jambo hilo.

Amma Mwanachuoni huyo yeye alikuwa akitetea shuraa kwa nguvu zote na pembeni yake lilikuwepo kundi la wanafunzi ambao wanachukua elimu kwake na wakimuunga mkono katika kila alisemalo kwa madai kwamba hoja zake ni kutoka ndani ya Qur'an Tukufu, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake (s.a.w.): "Washauri katika jambo." Na anasema tena: "Na jambo lao ni kushauriana kati yao."

Niligundua ya kwamba mimi ninashinikizwa na jamaa kwa kuwa wao wamejifunza kutoka kwa waalimu zao fikra zote za Kiwahabi, kama nilifahamu pia kwamba, wao hawawezi kukubali kusikiliza hadithi sahihi na wanang'ang'ania baadhi ya hadithi walizozihifadhi na nyingi ya hizo ni hadithi zilizozushwa (na kusingiziwa kuwa Mtume alisema hivyo) basi hapo nilikubaliana na msingi wa Shuraa nikawaambia wanafunzi hao na waalimu wao kama ifuatavyo:

"Je, hivi ninyi mnaweza kuitosheleza serikali ya Mtukufu Mfalme (wa Saudia) juu ya msingi wa Shuraa ulioko kwenu mpaka (Mfalme), ajiondoe kwenye utawala wake na afuate viongozi wenu bora waliopita na awaachie Waislamu hilo bara Arabu likiwa na uhuru wa kuchagua kiongozi wao? Mimi sidhani kama (Mfalme huyo) atafanya hivyo, kwani baba zake na babu zake hawakumiliki ukhalifa peke yake bali bara Arabu nzima pia imekuwa ni milki yao mpaka ardhi yote ya Hijazi wakaipa jina la Mamlaka ya Saudia.

Basi hapo ndipo aliposema mwanachuoni wao mkuu kuwa: "Sisi hatujishughulishi na mambo ya kisiasa, sisi tumo ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo ameamuru litajwe jina lake na paswaliwe ndani yake. Mimi nikasema: "Je, hali hiyo hata kwa msomi mwenye maarifa?" akasema: "Ndiyo, sisi hapa tunawafunza namna hiyo vijana. Mimi nikasema: "Sisi tulikuwa katika uchambuzi wa kielimu." Akasema: "Bila shaka wewe ndiwe uliyeuharibu (uchambuzi huo) kwa kuingiza mambo ya siasa"

Basi nilitoka hapo pamoja na niliokuwa nimefuatana nao hali ya kuwa ninawasikitikia vijana wa Kiislamu ambao uwahabi umetawala fikra zao kwa kila namna mpaka wakawa ni maadui wa wazazi wao. Wazazi wao wote ni watu wanaofuata madhehebu ya Shafii, madhehebu ambayo yako karibu mno na madhehebu ya watu wa nyumba ya Mtume kama ninavyoamini mimi, (kwani hapo kabla) Masheikh walikuwa na heshima na utulivu mbele ya wasomi na wasiokuwa wasomi hasa kwa kuzingatia kwamba wengi wa Masheikh hao ni Masharifu wanatokana na kizazi kitukufu, basi hatimaye wakaja Mawahabi wakawashinikiza vijana kutokana na ufakiri wao na wakawahadaa kwa mali na nyenzo za maisha. Wakaugeuza mtazamo wao (kwa kuwaambia) kuwa wayatendayo ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu Masharifu ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu kwani (heshima hiyo waifanyayo) ni kumtukuza kiumbe. Basi hapo ndipo watoto hawa wakawa ni kero na balaa kwa baba zao, na hali kama hii kwa bahati mbaya ndiyo inayotokea katika miji mingi ya Kiislamu katika Afrika.

Hebu na turejee kwenye kifo cha Abubakr, kwani tunamkuta kabla ya kufa kwake anajuta kwa yale aliyoyatenda. Ibn Qutaibah ameandika ndani ya kitabu chake kiitwacho, Tarikhul-khulafai kauli ya Abubakr anasema:
"Naam yamenifika, Wallahi sijuti isipokuwa kwa sababu ya mambo matatu niliyoyafanya, lau ningeyaacha mambo hayo nisiyafanye, Laiti mimi ningeiacha nyumba ya Ali, mapokezi mengine yanasema, Laiti nisingeifedhehesha nyumba ya Fatimah kwa jambo lolote lile japokuwa walikuwa wametangaza vita dhidi yangu, na laiti mimi ile siku ya Saqifah ya Bani Saidah ningeweka (mkono wangu) ndani ya mkono wa mmoja wao kati ya watu wawili, Abu Ubaidah au Umar akawa yeye ndiyo amir nami nikawa waziri, na laiti mimi pale o nilipoletewa Dhil-fujaat as-Sulami hali ya kuwa yu mateka, basi bora ningemuuwa kwa kumchinja au ningemuachia huru na nisinge mchoma moto.

Nasi tunaongezea hapo tunasema, "Laiti ewe Abubakr usingemdhulumu' bibi Fatmah na wala usingemuudhi na usingemkasirisha, na laiti wewe ungejutia kabla ya kufa kwake na umridhishe, hayo yanaihusu nyumba ya Ali uliyoifedhehesha na ukaruhusu ichomwe moto."

Ama kuhusu ukhalifa, basi laiti wewe ungewaacha jamaa zako ambao ndiyo nguzo zako (yaani) Abu-ubaidah na Umar na ukaweka mkono wako ndani ya mkono wa muhusika wake kisheria ambaye alitawalishwa na Mtume akawa yeye ndiye Amir!! Kwa kufanya hivyo ulimwengu huu tunao ushuhudia leo hii usingekuwa hivi, na dini ya Mwenyezi Mungu ingekuwa ndiyo inayoongoza ulimwengu kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu na ahadi ya Mwenyezi ni ya kweli.

Ama kumuhusu Al-fujat as-Sulami uliyemchoma moto sisi tunakwambia, "Basi laiti wewe usingezichoma moto Sunna za Mtume ambazo ulizikusanya, hapana shaka ungejifunza mengi kutokana nazo kuhusu hukumu za sheria zilizosahihi na wala usingetegemea jitihada ya maoni yako.

Na mwisho, tunakwambia ukiwa juu ya kitanda cha mauti "Laiti wewe ulipofikiria juu ya kuacha ukhalifa, ungelirejesha haki (hiyo) mahala pake kwa yule ambaye mahali pake katika ukhalifa ni sawa na mahali pa mpini wa jiwe la kusagia nafaka."

Na wewe unafahamu mno kuliko watu wengine juu ya ubora wake, ucha Mungu wake, elimu yake na kwamba yeye alikuwa kama nafsi ya Mtume (s.a.w.w.) na hasa kwamba yeye alikuachia jambo hilo na hakukupinga (yote hayo akikusudia) usalama wa Uislamu. Basi kwako kulikuwa na uhuru wa kuupa nasaha umma wa Muhammad (s.a.w.w.) na uuchagulie mtu ambaye atautengenezea mambo yake na kuuweka pamoja na akaufikisha kwenye kilele cha mafanikio.

Na tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akusamehe madhambi yako na amridhishe bibi Fatmah, baba yake, mumewe na wanawe, kwani wewe ulimkasirisha (binti ya Mtume) aliye sehemu ya mwili wa Mtume na Mwenyezi Mungu hukasirika kwa ajili ya kukasirika kwake na huwa radhi kwa kuwa radhi kwake, kama ambavyo mwenye kumuudhi Fatmah basi hakika huwa kamuudhi Baba yake kwa mujibu wa hadithi ya Mtume (s.a.w.), na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

''Wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, watapata adhabu kali." Nasi tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na ghadhabu za Mwenyezi Mungu, na tunamuomba aturidhie sisi na Waislamu wote wa kiume na wa kike na waumini wote wa kiume na wa kike.
Mwisho wa maudhui hii.

maoni

Acha Maoni

*Mashamba alama ya asteriski ni hakika kuwa thamani.