MAHDI (A.S) (3)

MAHDI (A.S) (3)

SEHEMU YA TATUUWEZEKANO WA KUGHIBU NA DALILI ZAKEImetuthibitikia kutokana na yote yaliyo tangulia kuwa fikra ya (kuja kwa) Mahdi, ni fikra iliyochimbuka kwenye sheria halisi ya kiislamu, na Mtume (s.a.w) alitoa bishara ya fikra hiyo katika hadithi zilizo kuja kutoka kwake, na wanazuoni wa hadithi tabaka kwa tabaka wakarithishana na kupeana riwaya hizo kama ilivyo thibiti vilevile ya kuwa Mahdi aliezungumziwa kwenye hadithi ni Muhammad bin Hassan Al-askari, na kwamba alizali-wa kwenye mji wa Sammarraa na habari za kuzaliwa kwake kujulikana kwa siku ile aliyo zaliwa kwa watu maalumu katika maswahaba wa baba yake, kisha akawa mashuhuri baada ya kuzaliwa kwake kwenye vitabu vya historia.

Na ni lazima kwetu baada ya kuthibitika sehemu mbili za mwanzo tuhamie kwenye maudhui ya sehemu ya tatu na ya mwisho inayo husiana na hatua ifuatiayo baada ya kuzaliwa Muhammad bin Hassan na kuthibiti kuwa yeye ndie Mahdi.

Na huenda ikawa bora zaidi ili kufuata mfumo maalumu na ili kuweka wazi jambo hilo, twende hatua kwa hatua kwenye mazungumzo yetu kufuatia mtiririko ufuatao:

01: Je Mahdi alighibu (alifichika na kutoonekana)?

02: Tukijaalia kuwa kuna uwezekano wa kughibu, je mtu anaweza kubakia akiwa hai kwa muda wa karne zote hizo?

Na ni vizuri kwetu, na huku tukiwa tumefikia sehemu nyeti na ya muhimu zaidi katika utafiti huu, tutangulize utangulizi ufuatao kabla ya kuingia kwenye kina cha maudhui yenyewe, ili utusaidie kufikia natija zilizo safi na malengo kuwa wazi.

Hakika Uislamu uliifanya akili kuwa ndio chimbuko la itikadi na msingi wa Imani, na ukakataa kufanya taklidi (kuwa-fuata watu ufuataji usio na dalili) na ufuataji wa kiupofu, na lengo la kufanya hivyo ni kuwa misingi ya itikadi na mizizi yake ijitege-meze kwenye akili na kuitegemea akili, na misingi hiyo ipate nguvu yake na kujizatiti kutokana na akili pekee, bila kushiriki kitu kingine chochote kwenye suala hilo kama matamanio ya nafsi na kutawaliwa na hisia za ndani na kufuata watu wengine.

Na hivyo ndivyo akili ilivyo kuwa ni dalili ya kumtambulisha Mwenyezi Mungu, nayo ndiyo iongozayo kwenye Imani. Katika kuwepo Mwenyezi Mungu na Umoja wake na katika ulazima wa kuwepo kwake, kisha akili vilevile ili kuwa ni dalili ya kuthibiti-sha ulazima wa kuwepo utume na uimamu na kuwepo marejeo ya kiama yakiwa ni matawi ya Imani ya Mwenyezi Mungu alie tukuka.

Ama maneno mengine ya hukumu za sheria na dalili za kidini hazihitajii dalili ya kiakili, na si lazima kwa mambo yao kusima-misha dalili kama hii, bali inatosha kulazimika kuyakubali kwa kutolewa tu dalili yenyewe ya aya au riwaya, juu ya suala hilo kwa njia za kisheria zilizo thibitisha ulazima wa kuzitii na kuzi-fuata dalili za kidini (aya na riwaya).

Kutokana na haya waislamu wakaamini kwa ukweli na kwa yakini, mas’ala ya kuwepo malaika kwa mfano, au kuamini kuwa Issa alizungumza akiwa mtoto mchanga au habari za mawe kumsabihi Mwenyezi Mungu yakiwa mikononi mwa Mtume (s.a.w), kwa ajili ya kuzungumziwa mambo haya kwenye Qur’an tukufu na sunna sahihi.

Na sisi tunapofanya utafiti kuhusu maudhui ya Mahdi na kughibu kwake tunayafanyia utafiti pamoja na waislamu wenye kukubali misingi ya uislamu na misingi ya sheria, bila ya kuwahusisha wengine wapingao kuwepo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu au ambao bado hawajawa waislamu, na kufanya hivyo ni kwa sababu mas’ala yenyewe yalivyo, yanategemea kutolewa dalili na ushahidi wa Qur’an tukufu na Sunna tukufu, kwa hivyo haifai kuyazungumzia mas’ala haya pamoja na mtu asie kiamini kitabu na sunna.

Kwa ibara nyingine, hakika sisi tunayafanyia utafiti maudhui haya juu ya msingi wa itikadi ya dini yenye kujitegemeza kwenye dalili za kisheria ambazo waislamu wote wamekubaliana na kuafikiana ya kuwa ni wajibu kuvifuata na kuvifanyisha kazi na si kwa kufuata msingi mwingine wala mas’ala haya kwa hali yoyote hayajawahi kuwa kama kazi ya kimahesabu ya kawaida kama jibu la 2×2 au kama kanuni ya kifalsafa ambayo haiwe-zekani kuzungumziwa na kujadiliwa kama kubatilika kwa dauru (mzunguko usio na mwisho) au tasalsulu (silsila ya vitu vyenye uhusiano isiyo kuwa na kikomo).

Kwa hivyo basi, na awe msomaji mtukufu ni mwenye kufaha-mu ya kuwa sisi tutayazungumzia na kuyafanyia utafiti mas’ala haya au tatizo hili kwa pande zake zote kwa kufuata msingi wa kitabu na sunna kwa sababu vitu hivi viwili ndio chimbuko la sheria na mlango wa maarifa na elimu kwa waislamu, na kwamba kuvipinga na kutoka kwenye msingi wa kuvifuata ni sawa na kuupinga Uislamu na kutoka dhidi ya hukumu zake na amri zake.[64]

Ukiwa wazi utangulizi huu, tunasema:

Hakika hadithi tukufu za Mtume ambazo zimepokelewa na mahufadh wa hadithi, na wakiwemo kati yao wale ambao waislamu wamekubaliana juu ya usahihi wa hadithi zao, zimekariri mara kadha neno la “kughibu”. [65]

Na kati ya hadithi zingine zinasema “Ataghibu”, kutakuwa na hali ya watu kutapatapa na kutahayari, na kaumu zitapotea kwenye hali hiyo”.[66]

Na katika riwaya nyingine:

)يغيب عن اوليائه غيبة،لا يثبت على القول بإمامته إلاَ من امتحن الله قلبه للأيمان(

Na katika riwaya nyingine “Ataghibu na kuto onekana kwa wapenzi wake, kuto onekana ambako hatabakia kwenye Imani na kauli ya Uimamu wake isipokuwa yule ambae Mwenyezi Mungu amempa mtihani moyo wake kwa Imani.[67]

Na katika hadithi ya Ibnu Abbas:

(يبعث المهدي بعد إياس،وحتى يقول النَاس:لامهدي) “Atatumwa Mahdi baada ya kukata tamaa, na mpaka watu waseme:Hakuna Mahdi”.[68]

Neno “ghaib” kama hadithi tulizo zitaja zilivyo,haina maana ya kumuhuisha Mahdi baada ya kufa kwake, na kumrejesha duniani baada ya kufa kwake bali hadithi hizo zina angalia kwenye ile hali ya kuto onekana kwake na kufichika kwake na watu kutomuona na kumshuhudia, na haya ndio yafahamikayo kwa haraka kwa kila msomaji pindi anapo soma hadithi hii na kulipima neno (ghaiba) lililo kaririwa kwenye hadithi hizo.

Na hadithi tukufu ambazo waislamu wamekubaliana juu ya riwaya yake.

(من مات Ùˆ لم يعرف امام زمانه مات ميتة جاهلية)“Mwenye kufa na haku-mjua Imamu wa zama zake amekufa kifo cha kijahili”. Hadithi hii iko wazi katika kuonyesha ulazima wa kuwepo Imamu katika kila zama na kila wakati.

Na baada ya kuthibiti kuzaliwa kwa Muhammad bin Hassan kwa dalili zisizo na shaka, neno “ghaiba” na ulazima wa kuwepo Imamu katika kila zama na kuwa ni dalili mbili za wazi zithibitishazo kuendelea kuwa hai kwa Mahdi kwa muda wa karne zote hizi na zinakuwa dalili za kupinga maneno mengine yasemayo kuhusu maudhui haya, maneno yenye kutilia shaka na kutowezekana kufanyika kitu kama hicho.

Na kauli ya kuwa Mahdi amekufa, pamoja na kuwa inapi-ngana na hadithi za ghaiba na hadithi za kuendelea kuwa hai kwa uimamu, hakuna mwana historia yeyote alieitolea ushahidi, na haikutajwa kwenye kitabu chochote ikiwa miongoni mwake vitabu vya wapingao suala hili… Amekufa lini? Na katika siku ipi na mwezi gani na mwaka gani na wakati gani, alipelekwa kuzikwa na ni akina nani walio hudhuria mazishi yake na amezikwa wapi na katika nchi gani??

Hakika yote haya yanatilia mkazo kuwa Mahdi, yuhai hakufa na kwamba yeye alighibu na kufichika mbali ya macho ya maadui zake, ili kuyahifadhi maisha yake na kuiokoa nafsi yake na kufichika kwake kulikuwa ni kwa aina mbili.Aina ya kwanza:

Kutoonekana kwa watu pale jeshi la khalifa walipo ivamia nyumba ya Imamu Askari baada ya kufariki kwake. Na katika kipindi hiki alikuwa akiwasiliana na mawakili wake na kuwapatia majibu juu ya maswali na matatizo ambayo mashia wakiyaele-keza kwake.

Aina ya pili:

Ni kutoonekana kwake kiukamilifu kwenye macho ya watu kiasi kwamba alikuwa hawasiliani na yeyote.[69]

Hakika suali la muhimu linalojitokeza kwenye akili, baada ya kuthibitika kuwepo kwa Mahdi na kufichika kwake na maisha yake kuendelea hadi leo, ni hili: Je anaweza kubakia hai kwa muda wa miaka yote hiyo? Na je, akili ina kubaliana na hilo?

Kabla ya kujibu swali hilo tunapenda kumkumbusha mso-maji yaliyo tangulia kusemwa kuwa, mambo ya kweli ya kisheria yakithibitika kwa habari za kunukuliwa zilizo sahihi, basi sisi kwa kuzingatia kuwa ni Waislam, ni lazima kwetu kufuata na kutii habari hizo na kuikubali hata kama akili zetu hazikupata njia na muongozo wa kufahamu falsafa yake na kujua siri zake.

Kwa hakika kutofahamu hekima ya hukumu hii au sababu yake, haiwi ni dalili ya kuipinga na kuikataa, bali ni lazima kusalimu amri na kutekeleza kwa hali yoyote, na haifai katika Uislamu, Muislamu kupinga hukumu moja wapo kati ya hukumu zake au kuitoa na kutolikubali suala lolote lililo elezewa kwa hoja ya kutofahamu siri au kutokinaika na sababu iliyotolewa.

Ama umri kuwa mrefu na maisha kuendelea kuwepo kwa muda wote huo kwa mamia ya miaka sio katika mambo yaliyo muhali, na kutowezekana kama wanavyo dhania baadhi ya watu bali imepokelewa riwaya na wana historia na kusimulia juu ya kutokea hilo kwa wingi, kwenye historia ya wanadamu ambayo ni ndefu. Kwa mfano Adam (a.s) alipewa umri na kuishi kwa muda wa miaka elfu moja. Na Lukman mwenyewe alipewa umri wa miaka elfu tatu na miatano (3500). Na Salman Al-faarsi (Mungu amuwie radhi) aliishi muda mrefu hapa aridhini, na baadhi ya wana historia wanadai kuwa aliishi zama za Masihi Issa (a.s) na kuudiriki Uislamu na akafariki kwenye zama za Khalifu Omar binil Khattab.

Na wengine wengi waliopewa umri wa mamia ya miaka na habari zao kusimuliwa na wanahistoria na hasa Assajastani alie kusanya habari zao kwenye kitabu alicho kiita “Al-muammarun” (waliopewa umri mrefu) kilicho chapishwa kwa mara ya kwanza Misri mwaka 1323 H, 1905 AD. Huu ni uthibitisho kwa upande wa kihistoria.

Ama Qur’ani tukufu ndio kauli iliyo ya kweli zaidi na hoja yenye nguvu zaidi kuliko mwana historia yeyote na riwaya yeyote.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu na kauli yake ni ya kweli: Hakika Nabii Nuhu (a.s.) alikaa katika kaumu yake akiwalingania kwenye Imani ya Mwenyezi Mungu kwa muda wa miaka “950” na Mwenyezi Mungu ndie ajuae ni muda gani alio ishi kabla ya kuanza wito na baada ya tuufani.

Na kwamba Mtume Yunusu (a.s) alibakia kwenye tumbo la nyangumi kwa muda mrefu na lau kama si fadhila za Mwenyezi Mungu wake angebaki kwenye tumbo lake hadi siku ya kiama.

(فلو لا انَه كان من المسبحين للبث في بطنه الى يوم يبعثون)“Basi isengelikuwa ya kwamba yeye alikuwa ni miongoni mwa wenye kumsabihi Mwenyezi Mungu bila shaka angekaa kwenye tumbo lake hadi siku ya kufufuliwa”.

Na maana ya kukaa huku ni kubakia kwake akiwa hai hadi siku ya kiama na nyangumi nae kubakia hai pamoja nae kwa muda wote huo ulio mrefu. Na kwamba watu wa pango (kahfu):

( لبثوا في كهف ثلاث مائة سنين وازدادوا تسعاَ) “Walikaa kwenye pango lao miaka mia tatu na wakazidisha tisa” wala hatufahamu ni kwa muda gani waliishi kabla ya kuingia pangoni na baada ya kutoka kwao.

Na kwamba:

)اوكالذي مر على قرية وهي خاوية على عروشها قال: أنى يحي هذه الله بعد موتها،فأماته الله مائة عام ثمَ بعثه،قال كم لبثت،قال لبثت يوماً أوبعض يوم،قال بل لبثت مائة عام،فانظر إلى طعامك وشرابك لم يتسنَه وانظر إلى حمارك(.

“Au kama yule ambae alipita kwenye kijiji (akakikuta) kikiwa kimeharibika na majumba yake kubomoka akasema:Vipi Mwenyezi Mungu anaweza kuvihuisha vitu hivi baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu akamfisha kwa muda wa miaka mia moja, kisha akamfufua akasema, umekaa hapa kwa muda gani? Akasema: Nimekaa kwa muda wa siku moja au nusu siku. Akasema: Bali umekaa kwa muda wa miaka mia moja, basi kiangalie chakula chako na kinywaji chako hakikugeuka wala kuharibika, na muangalie punda wako”.

Huwenda kubakia chakula na kinywaji (maziwa) kwa muda wa miaka mia moja bila kuharibika au kugeuka, ni jambo la ajabu zaidi kuliko umri mrefu wa mwanadamu na lengo lenye kustaajabisha zaidi.[70] Yote haya kwa kuongezea na mambo mengine waliyo yaandika waandishi wa historia na wana hadithi na wakayapokea kwa kuyakubali na kuhusu uhai wa Khidhiri ambae alikuwepo kabla ya zama za Mussa (a.s) na ataendelea kuwepo hadi zama za mwisho.

Je tuyaamini na kuyakubali yote hayo yaliyo zungumzwa na Qur’an na kupokelewa kwa wingi kwenye suna au la? Na je ina swihi kwetu kuyapinga na kuyakataa ilimradi tu akili ya mwanadamu kwa kiwango chake ilicho nacho haijaweza kufaha-mu siri ya mambo haya na bado haijaweza kufichua na kugundua mambo mengine yaliyo fichika na yasiyo julikana?

Maudhui ya kughibu kwa Mahdi mfano wake ni kama haya kiukamilifu, na ni lazima kwetu kukiri kuwa maisha na uhai wake ni wenye kuendelea kufuatia ushahidi na dalili hizo na kumswadikisha mtume (s.a.w) ambae “hatamki kwa matamanio yake bali ayasemayo ni wahyi ulio teremshwa” na kutekeleza amri yake Mwenyezi Mungu.

(وما اتاكم الرسول فخذوه) “Aliyo waleteeni Mtume yachukueni”, na imani yetu kwa vitu hivyo haitakuwa ni ajabu au jambo geni, au kuliamini jambo ambalo halijawahi kutokea kwenye Uislamu, bali kufanya hivyo ni sawa na kuamini umri mrefu wa Nabii Nuhu na kukaa kwa Yunusu kwenye tumbo la nyangumi, na kubakia kwa chakula na kinywaji (maziwa) kwa muda wa miaka mia moja bila kuharibika na bila kugeuka au kupatwa na uharibifu.

Na ikiwa dalili ya Qur’an na hadithi tukufu zimejulisha uwezekano wa mwanadamu kubakia hai zaidi ya miaka elfu moja na kutufahamisha kutokea hilo kwenye kaumu zilizo tangulia, basi hiyo haimaanishi kuwa jambo hilo liko juu ya uwezo wa kielimu na juu ya uwezo wa kiakili, na hii ni elimu ya kisasa inatueleza wazi ya kuwa mwanadamu anauwezo wa kubakia kwa maelfu ya miaka ikiwa ataweza kutayarishiwa nyenzo za kuzihifa-dhi nguvu za kimwili ambazo ndizo zimsaidiazo kubakia hai.

“Hakika maulamaa wenye kutegemewa kwa elimu zao wanasema: “Hakika chembe chembe za msingi kwenye kiwiliwili cha wanyama, zinakubali kubakia kwa muda mrefu usio na mwisho, na kuwa kuna uwezekano wa mwanadamu kubakia hai kwa maelfu kadha ya miaka ikiwa hakutokewa na vitu au vikwazo viwezavyo kukata kamba ya uhai wake, na kauli yao hii si dhana tu bali ni natija na matokeo ya majaribio (au kazi iliyo fanyiwa majaribio”.

“hakika mwanadamu hafi kwa sababu kuwa ameishi kwa muda wa miaka kadhaa, sabini au thamanini au mia moja au zaidi, bali kuna vitu vinavyo ingia kwenye baadhi ya viungo vyake na kuviharibu na kuto kuwepo mawasiliano kati ya viungu vyake vyenyewe na vyote vinakufa, na elimu ikiwa itaweza kuondoa vipingamizi vitokeavyo kwenye mwili au kuzuwia ufanyaji kazi wake au kuathirika kwake, hakutabakia kizuwizi kizuwiacho kuendelea kuishi mamia ya miaka”.[71]

Naye John Roston anaitakidi kutokana na ugunduzi na majaribio ya kielimu kuwa kufuata njia ya kumhifadhi mwana-damu, halijabakia kuonekana kuwa ni jambo muhali lisilo weze-kana[72], kwani ugunduzi ulio thibitishwa na kuandikwa na wana-zuoni na wataalamu mashuhuri tangu karne moja takriban unatupa na kutuachia matumaini ya uwezekano wa kufikia kufahamu na kugundua chembe zenye uwiano na chembe za mwilini zitakazo saidiana kuongeza kuishi kwa miaka mingi, kwa kutegemea majaribio ya kielimu aliyo yaandika Brown Sickward, Alexy Carl, Voronor, na Minsha bonkov na Bogau Molites,Vilator na wengineo”.

“Ama Robert Itinger, ambae aliweka mwishoni kitabu kizuri na makini kwa anwani “Je mwanadamu anaweza kubakia milele akiwa hai”, hakika alileta matarajio mapya pale alipo sema: “Hakika mwanadamu ambae anaishi na kupumua kwa hivi sasa anamiliki uwezo wa kubakia kwa upande wa kifizikia”.[73]

Haya yote ukiongezea na maneno mengine mengi yaliyo semwa wazi yaelezeayo uwezekano wa kuyahifadhi maisha ya mwanadamu kwa maelfu ya miaka ikiwa mwanadamu atagandi-shwa kwa kipindi hiki, kwa kuzingatia kuwa kugandishwa kunazihifadhi seli (chembe) zote za uhai, na wakati wowote inapotakiwa kumrudishia mwanadamu aliegandishwa ufanyaji kazi wa mwili wake hupewa au huwekewa kiwango fulani cha joto kilicho lazima kwenye mwili na kumfanya kurudi kwenye hali yake, kama alivyo kuwa mwenye nishati kwa harakati na mwenye uhai mwingi ndani yake.

Na vyovyote iwavyo, hakika maneno ya wazi ya wataalamu wa zama hizo yanasisitiza uwezekano wa umri wa mwanadamu kuwa mrefu, na kwamba uwezekano huo ndio kitu kikubwa kiwapacho msukumo juu ya kuendelea na kufanya juhudi za kutaka kuelewa nyenzo za vitu vinavyo weza kulifanya jambo hilo lifanikiwe.

Na ikiwa inafaa mwanadamu kuweza kurefuka umri wake kutokana na maandalizi na maumbile aliyo nayo, itakuwa ni jambo linalo wezekana umri wa Mahdi (a.s) kuwa mrefu kwa karne zote hizi kutokana na hali ya kimaumbile na utashi wa Mwenyezi Mungu.Na baada ya hayo:

Hakika wanadamu ambao wanaishi kwenye zama hizi ni wenye mazingira magumu sana ya kifikra na ambao ni wakati hatari sana wa utamaduni na wenye kuhitajia sana msuluhishaji huyu mwenye kutarajiwa na kusubiriwa, ambae ni lazima atoke siku fulani ili aweze kurudisha mwendo wa wanadamu kwenye njia au mfumo wake sahihi, na kumpitisha kwenye njia iliyo nyooka.

Bila shaka akili ya wanadamu, muislamu na asie muislamu, ikipata habari za mtu au msuluhishaji mfano wa huyo mwenye kungojewa, inakubali na kukiri kuwa ni lazima aje na ni lazima awepo, hata kama kusinge kuwa na dalili ya Qur’ani au hadithi juu ya mtu huyo au ishara juu ya mtu huyo. Bali hata mwana-falsafa wa Uingereza alie mashuhuri Bernard Show, alitoa bishara ya msuluhishaji huyo kwa msukumo wa fikra zake halisi na akaandika kitabu kuhusiana na hilo alicho kiita kwa jina la “Al-Insaan wa superman” na amesema kuwa msuluhishaji huyu mwenye kungojewa “ni mwanadamu alie hai mwenye ujenzi wa kiwiliwili ulio sahihi na uwezo wa kiakili wa kiwango cha juu sana kisicho cha kawaida, ni mtu wa kiwango cha juu sana na mtu huyu wa chini (yaani wa hali ya kawaida) atamfikia baada ya juhudi za muda mrefu” na kwamba yeye “umri wake utakuwa mrefu hata kuzidi miaka mia tatu, na anaweza kunufaika na vitu alivyo vikusanya kwenye zama zote hizo na alivyo vikusanya kwenye muda wote wa uhai wake ulio mrefu”.[74]

Na Abbas Mahmud al-a’qqad amesema akiongezea maelezo yake juu ya hilo: “Inatudhihirikia kuwa Superman show si jambo la muhali kuwepo na kwamba wito wake kwake haukosi ukweli ulio thabiti.[75]

Na hatuwezi kupata kheri mwishoni mwa mazungumzo hayo zaidi ya kumuelekea Mwenyezi Mungu na kumuomba kwa kuse-ma:“Ewe Mwenyezi Mungu, hakika sisi tunashitakia kwako kumkosa nabii wetu, na kughibu kwa mtawala wetu, na kuzidi kwa maadui wetu, na idadi yetu kuwa chache, na fitina (mitihani) kwetu kuwa mikali na zama kutugeuka na kushinda. Basi mrehemu Muhammad na (Aali) jamaa zake, na utusaidie juu ya hayo kwa ushindi wa haraka utokao kwako, na kwa kuondoa taabu na madhara na kwa ushindi uutukuzao, na utawala wa haki uudhihirishao”

“Ewe Mwenyezi Mungu mnusuru kwa nusra iliyotukufu, na umpe ushindi ulio mwepesi na utujalie tuwe ni katika wafuasi wake na wasaidizi wake, hakika wewe ni msikivu na mwenye kujibu maombi”.

“Na mwisho wa maombi yetu ni kuwa tunamshukuru Mwenyezi Mungu mola wa viumbe wote”.

***

NYONGEZABaada ya kutoka chapa ya kwanza ya kitabu hiki nilipokea barua kutoka kwa mheshimiwa Ustadh Muhammad Ridh’waan Al-Kasam kutoka Damaskas akipinga baadhi ya mambo yaliyo kuwemo kwenye bahthi yetu (utafiti).

Na ninafurahi sana kuelezea au kutoa shukurani zangu za dhati kwa Sheikh Al-kasam, kwa kutoa mwishoni mwa chapa hii baruwa yenyewe na jibu langu juu ya barua hiyo, huenda mso-maji mtukufu akapata ndani yake manufaa na faida fulani.Na Mwenyezi Mungu ndie atoae tawfiqi.***

BARUA YA SHEKH AL-KASAM.Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mwenye kurehemu.

Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe na rehma na amani ziwe juu ya Mtume wa mwisho.

Mheshimiwa Sayyid Muhammad Hassan Aalu Yaasin, Assalam alaykum wa rahmatullahi wa barakatuhu. Ama baada ya hayo.

Hakika nimesoma kitabu chako kiitwacho “Al-Mahdil-Muntadhar baina At-taswawuri wa At-tasdiiq” na uliyo yataja ndani ya kitabu hicho na kutokana na kauli yako kwamba ni utoaji wa habari ulio wa kweli na ni utoaji hukumu wenye amana na ni utafiti ulio safi ulio epukana na matamanio na mapenzi. Hakika jambo zuri lililo nistaajabisha kwenye kitabu hicho ni kauli yako kwenye ukurasa wa 50:

“Hakika Uislamu umeifanya akili kuwa ni chanzo cha itikadi na msingi wa Imani na ukakataza kufanya taklidi (kuwafuata watu fulani) ufuataji wa kiupofu “usio na ushahidi wala dalili”.

Nina sema ewe Sayyid mtukufu hakika kutokana na haya, ilikuwa haiwezekani kwangu isipokuwa kukutolea mambo ambayo ni lazima kuelezwa kati ya mambo niliyo yafahamu kutokana na masomo yangu, kwa kuzingatia kuwa ni mmoja wapo wa wafanyao kazi kwenye uwanja huo wa kiislamu ili kubainisha ninayo yaona ni sawa, na maelezo yangu ndio haya:

Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukataza moja kwa moja katika aya nyingi kuitakidi itikadi yoyote isiyo na yakini ndani yake na akasema “Sema je mna ujuzi wowote kuhusu hili mkatutolea”, na akasema tena “Kwa nini hawawaletei ushahidi ulio wazi, basi ni nani dhalimu zaidi kuliko aliemzulia Mwenyezi Mungu uongo”, na akasema tena “Hawana ujuzi wowote kuhusu suala hilo isipokuwa ni kufata dhana”.

Kwa hivyo yeye Mwenyezi Mungu anatutaka tuwe na ujuzi na maarifa na ushahidi na anatukataza kuwa na dhana na makatazo yake hayo anayaunganisha na ahadi na vitisho. Kutoka-na na hayo tunaweza kusema kuwa itikadi hazichukuliwi isipo-kuwa kutokana na yakini.

Na baada ya kukisoma kwa uchambuzi Kitabu chako na kuandika maoni yangu kukihusu, nimeona kuwa wewe umetaja kuwa fikra ya “Mahdi” imesimama juu ya msingi wa yakini na elimu au ujuzi ulio mutawatir na ukasema kwenye ukurasa wa “14”: “Kutokana na dalili za Mtume kuwa mutawatir katika haki ya Mahdi, mara kwa kueleza wazi na mara nyingine kwa kuashiria” na ukamalizia pembezoni mwa kitabu kuwa mtu anaweza kurejea kwenye kitabu muraja’ati cha Sheikh Sayyid Abdul-Hussen Sharafud dini na kitabu Al-ghadiir juzuu ya kwanza cha Al-Amiini.

Na kwa kurejea kwenye vitabu viwili hivyo hapakuwa ndani ya vitabu hivyo chochote kinacho faa kuwa ni dalili na ushahidi wa fikra hii, isipokuwa hadithi ambazo sanadi yake ni Auhaad (zisizofikia kiwango cha mutawatir) na si hadithi zilizo mutawa-tiri. Je hadithi sahihi zina kupatieni yakini katika nadharia yenu?

Hakika suala hili ni la kushangaza.

Kisha kuna jambo lingine ni vizuri kulitilia umuhimu nalo ni pale ulipo taja kwenye ukurasa “14” kama ifuatavyo: “Na ni-lazima ili kujiepusha na maovu haya awepo Imamu alie chaguliwa na mwenye sifa zote za ukamilifu, alie epukana na kutakasika na mambo yote yachukizayo, na alie mbali na kila aina ya uovu katika matendo na kutoka kwenye kanuni za sheria na hali hiyo ndiyo tuiitayo kwa jina la Isma” na kuendelea.

Ndugu yangu mpenzi, hiyo ni Ismah gani?

Je kuna mwanadamu yeyote mwenye Ismah basi utasemaje kuhusu kauli ya Mtume (s.a.w) isemayo “Kila mwanadamu ni mwenye kufanya makosa na watu bora (kati ya wafanyao makosa) ni wale wafanyao tauba (yaani waombao msamaha)”.

Je Mtume aliposema kila mwanadamu ni mwenye kukosea alimtoa kwenye hukumu hiyo mtu yeyote? Basi hoja na dalili ya Ismah iko wapi? Ukiongozea pamoja na haya kuwa wewe umetoa ushahidi wa hadithi sahihi ukurasa “53” “Mwenye kufa hali ya kuwa hakumfahamu Imamu wa zama zake amekufa kifo cha kijahili”, na ukafahamu kutokana na hadithi hiyo kuendelea kwa Uimamu wa Muhammad bin Hassan.

Ni mtu gani anae kubali kauli hii. Hakika sisi tunasema ya kuwa, hakika hadithi kwa matamshi yake na mafuhumu yake inasema kuwa ni juu ya kila muislamu kumfahamu Imamu wa zama zake, na ampe baia juu ya kukitekeleza au kukifuata kitabu na suna na haijulishi juu ya Imamu fulani maalumu.

Sasa kumuaminisha na kuufunga uimamu kwa maimamu kumi na mbili kumetoka wapi? Je si umeyasema hayo bila dalili?

Ikiwa tunamtaka Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, ni juu yetu kufuata dalili ya kidini, itakayo kuwa ni madhubuti tunachu-kua itikadi kutoka humo na hukumu, na itakayo kuwa ni yenye kutoa dhana tutachukua humo hukumu pekee, na haifai kwa muisilamu alie na ufahamu kamili abakie akiitakidi mambo yenye kudhaniwa na kuyaweka kwenye kiwango cha mambo ya itikadi bila kuwa na dalili na kusema kuwa Mahdi atakuja, na akaamini hivyo wakati ambapo hana dalili yoyote kati ya dalili za wahyi atakazo zitolea ushahidi juu ya kauli yake.

Na mimi ninatarajia kwa ndugu Ustadh na wafuasi wake watukufu kuwa maneno hayo niliyosema, yatulie na kukaa kwenye nafsi zao zilizo tulia ili kupata thawabu za Mwenyezi Mungu na radhi zake.

Wassalamu alykum warahmatullahi wabarakatuhu.

Damaskas, 15/Rabiiul-thani/89. (29/07/69).

MUHAMMAD RIDHWANI Al-KASAM.

JAWABU LA BARUAAssalamu alaykum warahmatullahi wa barakatuhu.Ama baada ya salamu,01: Bado nina sisitiza kauli yangu ya kuwa “Uislamu umeifa-nya akili kuwa ni chimbuko la itikadi na msingi wa Imani”, na mimi niko pamoja nanyi katika kusema kuwa “Itikadi hazichuku-liwi isipokuwa ni kutokana na yakini”, na sitorudi nyuma kuhu-siana na haya hata kidogo, sawa natija au matokeo ya hadithi hii yawe ni yangu au yawe juu yangu.

02: Hakika hadithi za Mtume kuwa mutawatiri kwa kuelezea wazi na kuashiria (tuliko kuashiria kwenye ukurasa wa 14 kwenye chapa ya kwanza) zina mhusu Ali (a.s) na kuwa yeye ndio Imamu wa kisheria baada ya kufariki Mtume (s.a.w). Na tumekusudia kwa neno mutawatiri, tawaturi ya kimaana na sio ya kimatamshi, na tunasema hivyo kwa sababu hadithi zote zilizo zungumzia suala hilo pamoja na kusisitiza kwake, zinaelekea kwenye suala la uimamu wa mtu huyu kidhati na kumuainisha, na lau kama hadithi ambazo sanadi yake inakuwa ni ya Aahaad[76], (kufuatana na ibara uliyotumia) zingeelekea kulielezea jambo moja pekee hakika bila shaka yoyote, jambo hilo litakuwa mutawaatir.

03: Tulifanya bahthi ya “Ismah” kwa upana kwenye kitabu chetu “Al-Imamah” na ninatarajia utakisoma na kunipa rai yako kwenye maudhui hayo.

04: Ama kauli yako isemayo “uteuzi na uainishaji na kulifu-nga jambo hilo kwenye idadi ya kumi na mbili, umetokea wapi? Na umekuja kutoka wapi? Je haya si umeyatowa bila dalili”? Utapata jibu lako kwenye kitabu “Al-Imamah” kilicho ashiriwa vile vile.

05: Ama uliyo yataja mwishoni mwa barua yako kuwa Mahdi ni miongoni mwa masuala yanayo dhaniwa ambayo haifai kuyapa daraja ya kuwa ni jambo la kiitikadi, hakika maneno haya ni dalili ya kuwa hukukisoma kitabu hicho kwa mazingatio, na lau kama ungerudia kukisoma ungeona majina ya maswahaba ambao wamepokea na kusimulia hadithi za Mahdi kutoka kwa Mtume (s.a.w) na majina ya wanazuoni ambao wametunga vitabu kuhusu Mahdi, na majina ya mahufadhi walio mashuhuri ambao wamezi-thibitisha hadithi hizi kwenye vitabu vyao, na ushahidi wa wahe-shimiwa wengi juu ya kuwa hadithi za Mahdi ni mutawaatir na kukata shauri juu ya usahihi wake.

Basi ni vipi yakini isithibiti na kukata shauri kwa yakini juu ya suala hili na kuwa na yakini kwa kuyashuhudia yote haya?

Na amani iwe juu ya mwenye kufuata uongofu na mwisho wa maombi yetu ni kuwa tuna mshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.***[1] Rejea kwenye kitabu chetu “Al-Imama”chapa ya Beirut mwaka 1392 H (1972 AD)

[2] Rejea sehemu yetu ya uimamu.

[3] Hii ni hadithi yenyewe ya mtume, ameitoa Ibnu Hajar Al-haitamiy katika Swawaiqul-Muhriqa ukurasa 99.

[4] Almahdi wal-mahdawiya cha Dr Ahmad Amin Ukurasa 110.

[5] Jarida la chuo kikuu cha kiislam Toleo la 3 ukurasa 161-162.

[6] Adabu Shiia ukurasa 101 na anayaunga mkono Dr Abdul-haliim Annajaar kwenye utangulizi wake wa kitabu Al Mahdiyyi fil-Islam. Hakika maulamaa wa hadithi wanasimulia kuwa fikra ya mahdy imefikia daraja ya kuwa mutawaatir kwa maana (yaani hadithi nyingi zimekuja kwa maana hii hata ingawa matamshi yametofautiana).

[7] Adaabu Shia:16.

[8] Wu’aadhu ssalaatwiin cha Dr Ali Al-wardu.

[9] Jarida la Atarbiyatul-Islamiyah/mwaka 14 toleo la 7/ukurasa:30.

[10] Alisimulia na kupokea kutoka kwake Ibnu Swabbagh Al Maaliky katika Alfusulul-Muhimma:275

[11] Amepokea kutoka kwake Al-haafidh Al-kanjii Asshaafii kwenye kitabu chake (Al-bayaan).

[12] Na kuna Nus’kha (kopi) iliyo chapwa na taasisi ya Ma’ahadul makhtutwatil- arabiya ya Kairo.

[13] Zimepokewa hadithi kutoka kwenye kitabu hicho katika As-afu-rraghiin:139, na kuna kopi zake zillizo andikwa kwa mkono katika mji wa Halab na Istambuli. Na ninayo kopi iliyo tolewa na kusomwa kwa mtunzi na iliyo hifadhiwa huko halab.

[14] Kuna kopi iliyo andikwa kwa mkono huko Istambuli.

[15] Mtunzi amekitaja kwenye kitabu chake “Al-aimatul-Itha ahar “,Uk:118.

[16]Kati ya vitabu hivyo viwili kopi iliandikwa kwa mkono iko Istambuli na ninayo kopi iliyochukuliwa kutoka kwenye asili ya kitabu cha

[17] “alburhani” kilichoandikwa kwa mkono na kilicho hifadhiwa huko Makka Mukarramah kwenye maktaba ya Haramul Makki.

5.Kitabu cha kwanza kopi ilio andikwa kwa mkono iko India na kopi ya Kitabu cha pili kiko Istambul.

[18] Kuna kopi yake iliyo andikwa kwa mkono Istambuli.

[19] Majalatul-jaamia Al-Islamiyah: Toleo 3/ukurasa 131.

[20] Al-ghadir 2/184 chapa ya najaf 1365 H.

[21] Al-ghadiir 2/223.

[22] Diiwaanu, Da’abul:42.

[23] Al-ghadiir 4/279.

[24] Matwaalibu ssaul 2/79.

[25] Sharhul-qawaid Assab’ul Alawiyat, Uk:70.

[26] Al-aimatul Ithna-ashar :118.

[27] Diiwan Abdallah bin alawiy iitwayo “Ad-duruhl-mandhum” Uk:18 na 146.

[28] Swawaiqul-muhriq:99. Na irejee “Al-Mahdi wal-mahdawiya”.

[29] Hassan ni sifa ya hadithi kutokana na wapokezi wake.

[30] Rejea kitabu Al-mahdi:9.

[31] Aswawaiqul-muhriqa:99 na Is-aafu-raaghibiin:243 na Al-hawiy 2/124.

[32] Sunanu Ibnu maja:2/1368 rejea Al-fusulul-Muhimma:276 na Yanabiul-mawaddah:435 na Al-hawiy:2/124

[33] Tadhkiratul-khawaas: 377. Na rejea Sunani Abi Daud: 2/422 na Swawaiqul muhriqa:98 na Nurul-Abswar: 156-157 na Al-hawiy :2/129-137

[34]Sunanu Abi Daud:2/422, na Aswawaaiqul-muhriqa:97 na Is-aafur-raghi-biin:131 na Al-hawiy:2/124

[35] Sunanu Abi Daud:2/422 na Aswawaiqul-muhariqa:97,na Nurul-abswar:157 na Al-hawiy:2/124-126 na katika Musnad Ahmad bin Hanbali 1/376 na 377-430-448 “Haitaondoka dunia au haitamalizika dunia mpaka awatawale waarabu mtu kutoka kwenye Ahlul-bait wangu,jina lake linafanana na jina langu”. Na mfano wa hadithi hii iko kwenye Sunan At-tirmidhi:4/505 na Tadh-kiratul-hufadh:2/488 na rejea Sunanu Ibnu Maaja:2/1366.

[36] Yanabiul-mawaddah:448 na Al-hawiy:2/190.

[37] Sunanu Abi-daud:2/422na Al-bayaan:64 na Swawaiqul-Muhriqa:97 na Is-aafur-raaghibiin:131, na Sunanu Ibnu Maaja:2/1368 na Al-hawiy:2/124 na 137.

[38] Yanabiul-Mawadda:455, na katika Al-bayaan:82 na miongoni mwa hadithi ya Mtume ambayo ni ndefu, Kisha akapiga kwenye bega la Hussen na kusema “Atatokana na huyu mahdi wa umma huu”.

[39] Yanabiiul-mawaddat:445.

[40] Yanabiul mawadda:441/445.

[41] Yanabiul mawadda:443 na Is-aaf Ar-raaghibiin:139-140.

[42] Kuhusu orodha hii rejea, kwa kuongezea vyanzo tulivyo vitaja hapo nyuma-bahthi ya Shekh Abdul Muhsin Al-abal kwenye majallatul-jaamiatul Islamyiyya toleo:3/128, nayo ina anuwani ya “Aqidatu ahlisunna wal-athar fil-mahdiy Al-muntadhar”.

[43] Majallatul jaamiatil-Islamiyyah Toleo:3/129.

[44] Al-Irhaad: 372 na Yanabiul-mawadda 451-452.

[45] Swahihu al-tirmidh :2/270 na Aswawaiqul-Muhriqa:97.

[46] Tadhkiratul-khawas:377 na matwalibus-saul:2/79 na Swawaiqul- Muhriqa :124 na Nurul Abswar:154.

[47] Alfusuulul-Ashara cha Shekhe Mufiid :13-14-.

[48] Alfusuulul-Ashara cha Shekhe Mufiid : 14

[49] Al-Irshaad:372.

[50] Al-Irshaad:372.

[51] Matwaalib As-sauli:2/79.

[52] Tadhkiratu-Khawaasi:377.

[53] Al-bayaan:102-112

[54] Wafiyatul-A’ayan:3/316.

[55] Al-wafiy bil-wafiyaat:2/336

[56] Aswawaiqul-muhriqa:124

[57] Al-fusulul muhimmah:274

[58] Al-aimatul-Ithna ashar:117

[59] Tuhfat Al-twalib :17/A (imeandikwa kwa mkono na iko kwenye maktaba ya Haram ya Makka katika namba 33/historia/Dahlawi).

[60] Is-aafur-Raghibiin:140.

[61] Yanabiul-mawaddah:450-451.

[62] Sabaik Adhahab : 78.

[63] Nurul-Abswar: 154.

[64] Na mambo ya ajabu sana aliyo yasimulia Dr Ahmad Amini kwenye kitabu chake “Al-Mahdi wal-mahdawiyat, Uk:108 kuhusu mas’ala haya alipo sema ya kuwa Madhehebu ya Ibnu khaladuni ni kukubali (Alkhabarul Wahid) habari moja (hadithi) ikiungwa mkono na hukumu ya akili, na kuzikataa hadithi nyingi ikiwa akili haikuziunga mkono na kwamba yeye alipinga kuwepo kwa Mahdi na fikra ya Mahdi kwa sababu fikra hiyo inapingana na hukumu ya akili yake!!

[65] Rejea Kitabu Al-bayan cha Al-haafidh Al-kanji Ashaafii:102-113.Na sheikh Kanduzi Al-hanafii kwenye yanabiul-Mawadda ametoa hadithi ukurasa:448 kutoka kwa Said bin Jubair kutoka kwa Ibnu Abbas (radhi za Allah ziwe juu yao) wamesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w):“ Hakika Ali ni wasii wangu na katika kizazi chake atatoka mwenye kusimama (juu ya haki) na mwenye kungojewa ambae ni Mahdi, ambae ataijaza ardhi kwa usawa na uadilifu kama ilivyo jazwa dhuluma na ujeuri. Nina apa kwa yule ambae amenituma kwa haki nikiwa mtoabishara na muonyaji, hakika wenye kusimama madhubuti juu ya kauli ya uimamu wake zama za kughibu kwake ni wachache zaidi kuliko baruti. Akasimama Jaabir bin Abdullah akasema:“ Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Je huyo mwenye kusimama kutoka kwenye kizazi chako atakuwa na ghaiba (atatoweka na kuto onekana)”?? Akasema Mtume: “Ndio, ninaapa kwa jina la Mola wangu, Mwenyezi Mungu atawachekecha wale ambao wameamini na atawaangamiza makafiri. Kisha akasema: Ewe Jaabir hakika hili ni jambo kati ya mambo ya Mwenyezi Mungu na siri kati ya siri zake Mwenyezi Mungu, jiepushe kuwa na shaka kwani kutia shaka kwenye jambo la Mwenyezi Mungu ni kufuru”.

[66] Yanaabiul-mawadda:488.

[67] yanaabiul- mawadda:495.

[68] Al-hawiy :2/152.

[69] Dr Ahmad Amin anawanasibishia mashia kuwa wao wana itakidi kuhusu Mahdi “ya kuwa pamoja na kuwa yuko mafichoni huwatia hamasa wafuasi wake ili waondoe dhuluma” na kwamba yeye anaishi mafichoni na huwaelekeza akiwa nyuma ya pazia kwa kuamuru na kukataza. Kitabu “Al-mahdy wal-mahdawiya” Uk:109na119 na vitabu vyote vya Shia vinasema wazi kuwa ameghibu na hawasiliani na yeyote, sasa ziko wapi kauli za kweli na iko wapi amana katika kunukuu habari?

[70] Pamoja na dalili zote hizi za Qur’ani zilizo wazi,hakika Dr Ahmad Amiin anaonelea kuwa mwanadamu “hawezi kufichika na akabaki mafichoni kwa mamia ya miaka bila Mwenyezi Mungu kumpitishia hukumu ya kifo”.Na akasema kuwa hilo haliwezekani“ isipokuwa kwa wajinga ambao wameondo-kewa na akili zao”. Al-mahdy wal-mahdawiya:96.

Je Dr Ahmad anaonelea kuwa kusadikisha suala la kutohukumiwa kwa kifo kwa Nuhu na Yunusu na Nyangumi na watu wa Kahfu (pango) ni dalili ya ukosefu wa akili?

[71] Majallatul-Muqtatwaf,mwaka wa 59/juzuu ya tatu.

[72]Kutumia neno muhali si sawa, na sawa ni kuwa haionekani kuwa ni jambo lililo mbali kufanyika.

[73]Jaridatul-ambaa Aljarida Albaghdaadiya, toleo namba:40/mwaka wa kwanza/27 march/mwaka:-1965 A.D. 1.Bernardshow, cha Abbas Mahmud Al-aqqad/Silsila ya Iq’rau/Tolea

[74] 89/Ukurasa 124-125.

[75] Kwenye kitabu hicho “Berardshow”.

[76] Aahaad ni hadithi ambayo sio mutawatir iwe imepokewa na mpokezi mmoja au zaidi.

maoni

Acha Maoni

*Mashamba alama ya asteriski ni hakika kuwa thamani.