MAHDI MTARAJIWA KATI YA TASWAWWUR NA TASDIQ

MAHDI  MTARAJIWA KATI  YA  TASWAWWUR  NA  TASDIQSuratu-Zukhruf:61 (وإنَه لعلم للساعة )“Na hakika yeye ni alama ya Kiama”.“Muqaatil bin Sulaiman amesema na wafasiri wengine wa Quran walio mfuata, hakika aya hii imeteremka kumhusu Almahdi”.

Ibn Hajar Al-haitami As-shaafii: Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:“Surat Aswaf:9” (ليظهره على الدين كله ولو كره المشركون)

“Ili aidhihirishe juu ya dini zote, hata kama washirikina watachukia”.“Said bin Jubair amesema : Ni Mahdi atokanae na kizazi cha Fatima (a.s)”.

Al-haafidh Al-Kanjiy As-shaafii.***

UTANGULIZIبسم الله الرحمن الرحيم

Kwa jinala Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema

Mwenye kurehemu.

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu kwa neema alizotoa na kutupa ilhaam. Na rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad na Ali zake wema.

Zilitolewa na kuzalishwa shub’ha na shaka kuhusu maudhui ya Mahdi mtarajiwa na kutawaliwa na majibizano, kati ya viku-ndi vya waislamu, hata baadhi ya waandishi na watunzi wa vitabu kufikia hatua ya kusema na kuona kuwa kumuamini Mahdi au fikra ya Mahdi ni sawa na kuamini mambo yaliyo pandikizwa yasiyo na ukweli au kuamini visa vya watu wa kale.

Kwa hivyo ilikuwa ni lazima kwa watafiti walio jihusisha na masomo ya kiislam, kutokana na hali hii, kuyaelekea na kuyafanyia utafiti maudhui haya, kwa kiwango kikubwa na kuyapa umuhimu mkubwa, na kuziandaa kalamu zao kwa ajili ya utafiti kuhusu masuala haya kwa uhuru kamili na uwazi, ili waweze kuondoa shub’ha zenye kutokea, na kuzibatilisha shaka zitokanazo na dhana, na kuyabatilisha madai yaliyo zuiliwa, na kuondoa pazia kwenye ukweli ulio wazi ili uweze kuonekana mbele ya watu wote kwa uhakika wake wa Uislamu au kama yalivyo kiuhakika wake ndani ya Uislamu wenye kumeremeta na kutoa mwanga.

Na huenda kati ya watu kuna wanao dhania kwamba kuyazungumziya maudhui haya na mengine mfano wake ni miongoni mwa mas’ala ambayo yanaweka kizuwizi cha kuleta ukaribu na kuelewana kati ya waislamu na kuchochea moto wa tofauti kati yao uzidi kuwaka na kulindima, na kwamba kuweka na kubakiza sitara au pazia kwenye mambo haya ni vizuri na ni jambo lenye manufaa zaidi, lakini kufikiria hivyo, kama ninavyo amini, ni dhana zisizo kuwa na ukweli na zisizo ufikia ukweli kwa aina yoyote, kwa sababu kuficha jambo haijawahi kuwa ni utatuzi wa matatizo kama haya, bali kufanya hivyo hakutatoa athari yoyote isipokuwa ni kuandaa mazingira mapana ya kupatikana dhana mbaya na kubobea hali ya kutofautiana na kuyachanganya mambo tofauti, kwa sababu hii kufanya utafiti wa makusudi kabisa kwa uwazi na ukweli ni jambo lenye athari ya upeo wa juu na lenye faida nyingi, kwani ukweli utadhihiri (uliokua haufaha-miki) na uongo wa kuunda na ulio zuliwa utakuwa wazi, na madirisha au nafasi za kutia shaka na kutoamini zitajifunga.

Na kutokana na haya, matarajio yangu kwenye kurasa hizi yalikuwa ni kwamba hizi kurasa ziwe hatua tuzifanyazo kwenye njia hii kuelekea kwenye lengo kubwa na ziweze kuwa juhudi zenye nia safi katika kujaribu kuleta mtazamo ulio salama na mafundisho yaliyo wazi na kuziba nyufa.

Na katika kijitabu hiki sintakuwa na nafasi kubwa -kwani kinaandikwa kwa msukumo huu mtukufu na kutaka kulithibi-tisha lengo hilo la juu kabisa- isipokuwa ni kuyadhihirisha kwa ukweli na kutoa hukumu iliyo salama, na kufanya utafiti ulio epukana na matamanio na mapenzi ya upande fulani.

Na matarajio yangu yote ni kuwa msomaji mtukufu apate ndani yake dalili zitakazo ondoa wingu jeusi ambalo limetanda juu ya maudhui haya kwa karne zote zilizo pita na apate dalili zinazo weka wazi msimamo wa Shia Imamiyya kuhusu mas’ala ya Mahdi na (kuhusu) fikira ya Mahdi.

Na himidi zote ni za Mwenyezi Mungu ambae alituongoza kwa hili, na hatukuwa ni wenye kuongoka lau kama si Mwenyezi Mungu kutuongoza.

Iraq-Al-KaadhimiyyaMUHAMMAD HASSAN AALU-YAASIN.***Muhtasari wa maudhui tuliyo yamaliza kwenye utafiti wa “Uimamu”[1] ni kuwa Uimamu kwa hukumu ya Hadithi, Qur’an na Akili ni sehemu ikamilishayo ujumbe, na ni sehemu iufanyayo ujumbe wa kiislamu uendelee kuwepo, na kwamba dalili zote zilizo julisha ulazima wa kuwepo utume na uwajibu wake zinafaa kuzinukulu na kuzitumia kutolea dalili juu ya ulazima wa kuwepo uimamu, kwa sababu kuwepo kwa utume bila ya uimamu ni kuwepo kuliko katika kusiko endelea, na hali hiyo inapingana na jengo la Uislamu lililo simama juu ya msingi wa kuendelea ujumbe hadi siku ya mwisho.

Kwa hivyo basi utume ni mwanzo wa uhai, na uimamu ni kuendelea kwa uhai ule na lau kama ingefaa kwetu kusema na kukubali utume bila uimamu, ingefaa kusema kuwa ujumbe wa Mtume una mtazamo finyu na wenye mipaka maalumu, hauku-weza wenyewe kujikadiria umri wa kuendelea kuwepo baada ya uhai wa Mtume wake, na haukuweka akiba kwa ajili ya kuyathi-bitisha malengo yake kwa kumteua Wasii ili aendeleze kazi na kuwepo kwa ujumbe wake.

Na ukweli ni kwamba, lau kama usia usingethibiti kutoka kwa Mtume (s.a.w) kwa njia ya riwaya na habari zilizo nukuliwa, hakika akili pekee ni yenye kuhukumu ulazima wa kuwepo usia na kuwa ulifanyika, na kwamba mtu yeyote miongoni mwetu haridhii kughibu na kuacha mali zake ziwezazo kutoweka au kufa na kuacha vitu mbali mbali hata kama ni vichache, bila kuzikabidhi mali hizi au zile kwa mtu alie muusia na muaminifu aziendeshe na kuzipangilia na kuzilinda.

Basi je ina juzu kwa Mtume wa Uislamu kuuacha urithi wake mkubwa, urithi ambao ni wa watu au wanadamu kwa zama zote, bila kumuweka wasii atakae uchunga na kuulinda urithi huu na kuuangalia kama inavyo stahili?!

Hakika mazingira yote yaliyo uzunguka Uislamu siku au wakati alipo fariki Mtume (s.a.w) yanatuita na kutulingania kuamini kuwa Mtume aliusia, na kwamba hakuliacha pandikizo lake lenye baraka jangwani, lipigwe na upepo mkali au joto kali lenye kuunguza au tukio lenye kulitokea, na kulifanya litoweke. Na hivyohivyo ina dhihiri wazi kuwa Shia Imamiyya hawakutoa maneno yahusianayo na kupinga kwao uchaguzi kutokana na hisia ya chuki kwa mtu fulani, au kutokana na rai yao ya kisiasa kwa maana ifahamikayo na yenye kuenea ya siasa, bali waliona kwenye Qur’an na Hadith dhamana sahihi ya maisha na nyenzo ya ujenzi iliyo salama, na basi wakawa wamevutiwa katika kuunga mkono rai hii kwa roho ya imani juu ya Uislamu na ikhlasi kwa ajili ya malengo na kuhisi maslahi ya Uislamu.

Ali bin Abi Twalib (a.s) alikuwa ni Imamu wa kwanza alie thibitishwa kwa dalili kwani riwaya za Mtume (s.a.w) ni nyingi sana nani “mutawaatiri” kumhusu yeye, baadhi zikimuelezea wazi na zingine zikimuashiria. Na riwaya zote hizo pamoja na kutofautiana matukio yake na minasaba yake na mifumo yake zinalenga, kama tulivyo tangulia kusema, kwenye kitu kimoja nacho ni kumteua mwenye cheo cha uimamu na ukhalifa baada ya kufa kwake Mtume (s.a.w).

Na imamu wa pili alikuwa ni Hassan bin Ali . Na watatu ni Hussen bin Ali. Na wa nne ni Ali bin Hussen Assajad. Na wa tano Muhammad bin Ali Albaaqir. Na wa sita ni Jaafar bin Muhammad Asswadiq. Na wa saba Mussa bin Jaafar Al-kaadhim. Na wa nane Ali bin Mussa Al-ridhaa. Na wa tisa Muhammad bin Ali Al-jawaad. Na wa kumi ni Ali bin Muhammad Alhaadi. Na wa kumi na moja ni Al-Hassani bin Ali Al-askari. Kisha alikuwa Muhammad binil-Hassan al mahdi ndie Imamu wa kumi na mbili[2], na alighibu kwenye macho ya watu hadi Mwenyezi Mungu atakapo toa idhini ya kudhihiri kwake na “kuujaza ulimwengu kutokana na yeye, uadilifu na usawa kama ulivyo jawa na dhuluma na ujeuri”[3].

Na mishale ya kutuhumu na kupinga ikamuelekea Almahdy kwa nguvu zote na kwa kutia mkazo na kusisitiza, na maneno yakawa mengi kwenye maudhui haya ya ghaiba (kufichika na kutoonekana) hadi kufunikwa na mawingu mazito ambayo hayakuwezeshi kuona na kufahamu na kukupa uwezo wa kudadisi na kupambanua lililo sahihi, na watafiti wengi ambao ni wenye ikhlasi wakajiweka kando na maudhui haya kwa kuyakimbia matatizo yake na ugunu wake, na sauti za wapingaji zikaja juu na kusikika kwa kudhalilisha na kufanya istihizaa nazo zikidhania kuwa silaha yake iliyo simama kwenye msingi wa kufanya maskhara na kutoa hila kuwa ni silaha kali yenye kukata isiyo katwa na wala haishindwi.

Na hivyo ndivyo utafiti wa “Almahdi na fikra ya kuwepo Almahdi” ulivyo jitenga na kuwa mbali na mfumo wa kielimu ulio salama. Na ukawa si utafiti wa kimaudhui wenye amani na ikhlasi, na ukawa chini ya msukumo wa mapenzi ya nafsi yaliyo mbali na akili na mantiki.

Na kutokana na hayo ilikuwa mfumo wetu kwenye kijitabu hiki ni lazima ufuate upande na mfumo usiofuata mapenzi na uwe ni mfumo wa kimaudhui, ili tujiepushe na tofauti ambazo wengi walizitumbukia. Na mfumo huu utasimama juu ya msingi wa kuyagawa mazungumzo hayo sehemu tatu .

Sehemu ya kwanza inakusudia kuitoa fikra yenyewe ya (Mahdi) na jinsi mahusiano yake na Uislamu yalivyo, na sehemu ya pili inaelekea kumuonyesha na kumuainisha (Mahdi) kwenye dalili zilizo pokelewa za Mtume, na sehemu ya tatu inazungumzia maudhui ya uwezekano wa kughibu na kutoonekana, na dalili zake.

Na mwendo huu ulioandaliwa na ufanyao uchunguzi, kama ninavyo itakidi, utachukuwa dhamana ya kutoa ufafanuzi na kuweka wazi kiukamilifu mambo yatakavyo gundulika na kupatikana kwenye mwendo huu na matokeo yake, na kutoa ufahamu makini wa matatizo yake kwa uhakika wake na ukweli wake wa asili ulio mbali na mapenzi na matamanio na malengo mengine.

SEHEMU YA KWANZAFIKRA YA KUWEPO KWA MAHDILau kama tutavitupia jicho la haraka vyanzo vya historia, na hasa historia ya dini mbali mbali, tungeweza kuelewa na kuona kwa uwazi kuwa kumuamini au Imani ya “Mahdi” sio jambo lihusikanalo na shia Imamiyya tu na sio katika mambo ambayo haya kuwepo kwenye dini na wao wakalizuwa, kama wasemavyo baadhi ya waandishi, bali jambo hilo sijambo lihusikanalo na waislamu peke yao na kutowahusu watu wengine wafuatao dini mbalimbali za mbinguni. Bali ukweli ni kuwa mayahudi na wakristo wana itakidi kuwepo kwa msuluhishi mwenye kutara-jiwa kuja katika zama za mwisho nae ni Eliya kwa mayahudi na Issa (Yesu) mwana wa Maryam kwa wa Kristo.

Kama ambavyo waislamu kwa ujumla, pamoja na madhehe-bu yao na vikundi vyao tofauti tofauti wanaamini hivyo kwani Shia Imamiyya (Ithina asharia) na kiisaniyya na Ismailiyya, wao wana amini kuwepo kwa “Mahdi” na wanasema wazi kuwa hilo ni katika mambo ya lazima ya madhehebu yao. Nao masunni wameamini vivyo hivyo (kuwepo kwa Mahdi) kwa kushikamana na rai hiyo kupitia maimamu wa madhehebu zao na wapokezi wao wa hadithi na baadhi yao wakadai kuwa wao ni akina Mahdi kama ilivyotokea Morocco, Libya na Sudan.

Na hivi ndivyo dini tatu za mbinguni (Uislamu,Ukristu na uyahudi) zinavyo kutana katika kuamini fikra hii ya Mahdi.

Na hivyohivyo mashia wanakutana na ndugu zao waislamu kwenye suala hili. Na wanaitakidi kuhusu Mahdi, mambo aliyo yasimulia Dr. Ahmad Amiin katika rai za masuni kuhusu huyo Mahdi kuwa“ Yeye ni katika alama za kiama, na kwamba ni lazima adhihiri kwenye zama za mwisho mtu atokanae na kizazi cha Mtume, atakae iendeleza dini na kudhihirisha uadilifu na waislamu watamfuata na atayatawala madola ya kiislamu, na anaitwa Al-mahdi”.[4]

Na kwamba rai yao kuhusu suala hilo ni kama rai ya Sheikh Abdul-Azizi bin Baaz, raisi wa chuo kikuu cha Kiislamu cha Madina pindi alipo sema:“Hakika suala la Mahdi ni suala lenye kueleweka na hadithi kuhusu suala hilo ni mustafiidha (zimepo-kewa na wapokezi watatu kwenye kila tabaka) bali ni mutawaatir (wapokezi wake ni wengi sana) na zenye kuungana…, nazo kwa ukweli kabisa zina thibitisha kuwa kuja kwa mtu huyu alie ahidiwa, ni jambo lililo thibiti na kutokea kwake ni jambo la Haki”.[5]

Na kutokana na haya hakika fikra hii (fikra ya kuja kwa Mahdi) yenyewe ni sahihi kama asemavyo muandishi wa Misri wa zama hizi aitwae Abdul-Hasiib Twaha Hamud.[6]

Lakini la kustajabisha na kuchekesha kuhusu suala hili, ni kuwa Abdul-Hasiib huyu hakugundua pale alipo isahihisha fikra hii kama ilivyo tangulia, ya kwamba alijipinga yeye mwenyewe, na alisahau kuwa alishawahi kutoa kauli ya kuwa:“Fikra ya Mahdi ni mojawapo kati ya matunda ya itikadi za (dini ya) Sabaiyyah”[7], nae kwa kusema hivyo anakusudia kuwa fikra hii imechukuliwa kutoka kwenye itikadi za mayahudi na haina mahusiano yoyote na Uislamu, hata ingawa hakusudii kwenye ibara yake hii isipokuwa kuwatuhumu Mashia ya kuwa wamechu-kua itikadi zao kutoka kwa mayahudi na kuwa hazina mahusiano yoyote na dini ya Kiislamu lakini kwa hakika amewatuhumu waislamu wote bila ya kutambua, kwa tuhuma mfano huo, na akazizingatia na kuzihesabu fikra alizoziita kuwa ni fikra sahihi hapo mwanzo kuwa ni moja wapo kati ya matunda ya itikadi za sabaiyyah, na huku ni kupingana kimaneno na kutetereka. Na ikiwa yatatujulisha juu ya jambo lolote maneno hayo, hapana shaka yanatujulisha nia mbaya na maradhi ya nafsi aliyo nayo, na hasa ukizingatia kuwa utafiti wa kihistoria wa zama zetu hizi umethibitisha kuwa hakuna mtu alieitwa Abdullah bin Sabai na kwamba huyu ni mtu alietengenezwa katika akili na kuundwa na akapambwa na kupewa sifa za kuwa ni mtu muhimu, na ana fikra fulani na ndie muwekaji wa itikadi na rai kadha, na huenda wale watu ambao walikuwa wakilirudia mara kwa mara jina la Abdullah bin Sabai mwanzoni mwa Uislamu walikuwa wakiku-sudia swahaba mtukufu Ammar bin Yaasir, kama wasemavyo baadhi ya watafiti.[8]

Na vyovyote iwavyo hakika natija ipatikanayo kutokana na utafiti wa kina na ulio safi usio na uchafu ni kuwa, Shia hawaku-zua fikra ya Mahdi, na wala hawakufuata itikadi ya dini ya Sabaiyyah au dini nyingine isiyo kuwa ya Sabaiyya, bali ni kwamba fikra ya kuwepo Mahdi ni fikra iliyo bashiriwa na dini tatu za mbinguni (Uyahudi, Ukristo na Uislamu), na kwamba Uislamu ulipotilia mkazo juu ya ukweli wa kielimu wa fikra ya Mahdy waislamu walifanya haraka kuikubali na kuinukulu na kusalim amri mbele ya fikra hiyo kwa kukubali kikamilifu.

Na haiwezekani yote haya yawe ni kunyenyekea kwa kitu kiitwacho kwa jina la “upotovu wa Shia na bidaa zao”, bali ni kukubali na kunyenyekea kuliko sahihi kwenye ukweli utokanao na itikadi za Kiislamu na hadithi za Mtume (s.a.w).

Na mwanazuoni mtukufu wa kisuni wa Iraq, alitoa muhtasari wa ukweli huu aitwae Sheikh Swafau ddin Aalu-Shaykh Al-halkah na akasema: “Ama Mahdi mtarajiwa, hadithi zilizopoke-lewa kumhusu zimefikia kiwango kikubwa na ni zenye kutuachia matumaini kwamba huyu atakuwapo zama za mwisho, na ataurudishia Uislamu usalama wake na imani, atairudishia nguvu yake, na dini atairudishia uzuri wake…, nazo ni hadithi muta-waatir bila shaka yoyote wala shub’ha, bali inasihi kutumia sifa ya mutawaatir kwa zinginezo zilizoduni yake, kufuatana na istilahi zote zilizo andikwa kwenye elimu ya Usuul”.

Ama athari tuzipatazo kutoka kwa maswahaba, zisemazo wazi kuwepo kwa Mahdi, ni nyingi sana zina hukumu ya Raf’u (kuinuliwa hadithi bila kutaja baadhi ya wapokezi).

Hakika hadithi alizo zitaja Al-barzanji kwenye kitabu cha Al-isha’ah Liasharaatisaa’a, na Aalusi kwenye Tafsiri yake, na Tirmidhy na Abu Dawud na Ibnu maaja na Alhakim na Abu ya’ali na Tabaraan na Abdur-rrazaaq na Ibn Hanbali, na Muslim, Abu Naiim, na Ibn Asakir, na Bayhaqiy, na Al-khatiib kwenye historia yake na Daruqutniy na Rady aany, na Naiim bin Hamad katika kitabu Alfitan na Ibnu Abu Sh’eiba na Abu Naiim Al-kuufiy, na Al-bazzaz, na Dailamiy na Abdul-Jabbar Al-khul’aniy kwenye Kitabu chake cha historia, na Aljuwainiy na Ibnu Habban na Abu Amru Addamiy kwenye sunani zake, katika yote hayo kuna dalili za kutosha.

Kwa hivyo kuamini kutokea kwa Mahdi ni waajibu, na kuitakidi kudhihiri kwake ni kuzikubali na kuziswadikisha hadithi za Mtume (s.a.w).[9] Na wanazuoni wengi wa kiislamu walifanya haraka kukubali na kukiri fikra ya Mahdi na kuzisahihisha habari zake kwa kutunga vitabu na vijitabu vya kutoa fat’wa na kufutu mas’ala katika maudhui hayo ili vizazi vijavyo viweze kufahamu suala hili na ukweli wake kama ilivyo pokelewa kwenye sheria kupitia kwa Mtume Mtukufu (s.a.w) na miongoni mwa waandishi hao wa maudhui haya, tukitaja baadhi kwa mfano, walikuwa ni:

1- Ubad bin Yaaqub al-rawajiniy alie kufa mwaka 250H. Ana kitabu kiitwacho “Akh’baarul-Mahdi”.

2- Abu naiim Al-Isbihaaniy alie fariki mwaka 430h. Ana kitabu kiitwacho “Ar-baina hadithan fi amril-Mahdi”[10] na kitabu “Manaaqibul Mahdi”[11] na kitabu “Na’atul Mahdi”.

3- Mohammad bin Yuusuf Al-Kanjy Ashaafiiy aliefariki mwaka 658 H, ana kitabu kiitwacho “al-bayaan fi akh’bari Swahib zzamaan”, kimechapishwa.

4- Yuusuf bin yahya Assalmy Ashaafiiy alie fariki mwaka 685 H. Ana kitabu kiitwacho “Uqad-Addurar fi Akh-baaril Mahdiyil Muntadhar”.[12]

5- Ibnu Qayyim Al-jauziya aliefariki mwaka 751 H, ana kitabu kiitwacho “Al-Mahdiy”.

6- Ibnu hajar Al-haitamy Ashaafii alie fariki mwaka 852 H, ana kitabu kiitwacho “Al-qaulul-mukhtasar fi alaamatil Mahdiy-Almuntadhar”.[13]

7-Jalaalu ddin Asuyutwiy alie fariki mwaka 911 H, ana kitabu

“Al-urful-wirdiy fi akhabaril-Mahdy” kimechapishwa na kitabu “Alamaatul-Mahdi”

8- Ibnu Kamaal basha Al-hanafi aliefariki mwaka 940 H, ana kitabu “Tal-khisul bayan fi alaamat Mahdiyyi Aakhiriz -zamaan”.[14]

9- Mohammad bin tuuluun Ad-damash-qi alie fariki mwaka 952 H, ana Kitabu “Al-muhdi ila ma-warada fil Mahdi”.[15]

10- Aly bin Hussaamud-din Al-mutaqiy Al-hindiy alie fariki mwaka 975H, ana kitabu “al-burhaan fi alaamati mahdiy Aakhiriz-zaman” na kitabu “Talkhiisul-Bayaan fi akhbari Mahdiy Aakhiriz-zaman”.[16]

11- Ali Al-qaariy Al-hanafiy aliefariki mwaka 1014 H, ana kitabu “Arrad alaa man hakama wa qadha annal Mahdy jaa’a wa madhwa”.

Na kitabu “Al-mashrabul-wirdiy fi akh-baril Mahdy”.[17]

12- Mar-ii bin Yusuf Al-Karamiy Al-hanbaliy alie fariki mwaka 1031 H, ana kitabu “Faraidu-fawaidul-fikri fil Imamil-Mahdiyil-Muntadhwar”.[18]

13- Al-Qaadhi Muhammad bin Ali Ash-shaukani alie fariki mwaka 1250 H, ana kitabu “Ataudhihu fi tawaturi majaa’a fil Mahdiy Almuntadhar wad-dajaali wal-masiih.[19]

14- Rashid Arrashid Atadhafiy Al-halabiy wa zama hizi ana kitabu “Tanwiir Ar-rijaal fi dhuhuril-Mahdy wa dajjal” kime chapishwa.

Hivyo hivyo washairi walikuwa pamoja na “fikra ya mahdi” na “Mahdi mwenyewe”, kwani kaswida zao zilikuwa na madhumuni na maana yaelezayo fikra hiyo na ambao ni wengi, na kaswida zao ni zenye kuelezea kutarajiwa kutokea siku yake, na kukiri kuja kwake kusiko na shaka na miongoni mwa washairi hao kwa mfano na kama ushahidi na sio kuwataja wote ni:

1- Al-Kumeit bin Zaid Al-asadi, aliefariki mwaka 126 H, na kuhusu suala hilo anasema:“Ni wakati gani itasimama haki kwenu na wakati gani atasimama Mahdy wenu wa pili.[20]

2- Ismaa’il bin Muhammad Al-himyari alie fariki mwaka 173H, nae anasema kuhusu hilo“Ni kwamba Bwana wa utawala na mwenye kusimama (na kuleta mabadiliko) ambae nafsi yangu inamuelekea kwa kuimba, anayo ghaiba, ni lazima aghibu. Basi Mwenyezi Mungu amrehemu mwenye kughibu, atakaa kipindi fulani kisha atadhihiri kipindi kingine, na kuujaza uadilifu mashariki yote na magharibi”.[21]

3- Da’abal a-Khuza’iy aliefariki mwaka 246 H, anasema kuhusu hilo:“Kutoka kwa Imamu hakuna shaka atatoka. Atasi-mama juu ya jina la Mwenyezi Mungu na baraka zake, na atatu-pambanulia haki na batili na atatoa malipo kwa neema na adhabu.[22]

4- Mihyaar-Ad-daylamy aliefariki mwaka 428 H, anasema kuhusu hilo:“Huenda zama za kesho zikaiponya mioyo ya wenye ghadhabu kutokana na wenye kukufanyia uadui.

Huenda ushindi wa haki ukawa juu ya jambo lisilo wezekana, huenda upungufu ukashindwa na utukufu na ubora kwa kusikia kwangu wito wa huyo mtu wenu atakae simama akiitikiwa na kila mwenye kuomba msaada.

5- Ibnu Muniir Attaraabilsiy aliefariki mwaka 548 H, amese-ma kuhusu hilo kwa njia ya mzaha na utani “Nimewatawalisha watu wa kizazi cha umayya walio safi watukufu na walio barikiwa na ninamkadhibisha mpokezi na ninatia ila kwenye kudhihiri kwa Mahadi”.[23]

6- Muhammad bin Twalha Ashaafiy aliefariki mwaka 652 H, anasema:“Na alisema Mtume (s.a.w) kauli tuliyo ipokea”. Akaendelea hadi kusema “ Na hakika alimdhihirisha kwa kueleza nasaba yake na sifa zake na kumuita jina lake, na inatosha kauli yake kuwa “anatokana na mimi” kudhihiri uhai na maisha yake na katika pande la nyama yake ni Zahra ndio mahala pake na sharafu yake watakao sema ni Mahdi hawa kukosea kwa hilo walilo litamka”.[24]

7- Ibnu Abil-hadiid Al-Mu’utazilii alie fariki mwaka 656 H, amesema kuhusu hilo: “Hakika nimefahamu ya kuwa ni lazima aje Mahdi wenu, na siku ya kuja kwake ninaitarajia. Atahudu-miwa na vikosi vya jeshi la Mwenyezi Mungu, kama mtu mwenye maumivu amekuja akiwa ni mwenye ushindi na kikisonga mbele kizazi cha Abil-hadidi wa kiwa mashujaa na walio mashuhuri na mikuki iliyo inuliwa juu.[25]

8- Shamsud-din Muhammad bin Tuulun Al-Hanafy Ad-damsh-qiy aliefariki mwaka 953H, anasema kwenye kasida yake akiyataja majina ya Maimamu kumi na wawili:“Na Askari Hassan alietwahirika Muhammadul-Mahdi atadhihiri”.[26]

9- Abdullah bin Alawi Al-hadaad Attarimy Ashaafi’i, alie fariki mwaka 1132 H, na kuhusiana na hayo amesema: “Muhammad Al-mahdi ni khalifa wa Mola wetu, Imam wa uongofu na dola lake linasimama kwa uadilifu kana kwamba namuona (siku hizo) akiwa baina ya maqaam na nguzo yake (yaani kati ya nguzo ya kaaba na maqam ya Ibrahim) wakimpa baiya kila upande wenye kumpongeza”. Na anasema katika sehemu nyingine: “Na kwetu kuna Imam umefika wakati wa kutoka kwake, atasimama kwa amri ya Mwenyezi Mungu kama ipasavyo, na kuujaza ulimwengu kwa haki na uadilifu na uongofu, kama ulivyo jazwa jeuri kwa dhulma ya watu waovu.[27]

maoni

Acha Maoni

*Mashamba alama ya asteriski ni hakika kuwa thamani.