HOJA ZA MAULIDI YA MTUME (S.A.W.W)

HOJA ZA MAULIDI YA MTUME (S.A.W.W)

Katika hujja yao ya tano wanasema: Hakuna ushahidi wowote, wa Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.), unaothubutisha usawa wa kuyasoma maulidi, sikwambii kuyatilia nguvu.

MAJIBU YETU: Katika majibu yetu ya hujja yao ya pili, tulieleza kwamba -- kwa mujibu wa msingi mmoja kati ya misingi muhimu ya sharia ya Kiislamu -- anayetakikana kuthubutisha kuwa maulidi hayafai kusomwa si anayesema yasomwe; ni anayesema yasisomwe. Kwa hivyo ushahidi wa Qur'ani na Hadithi unaotakikana si wa kutolewa na sisi tunaosema ni sawa kusoma maulidi, bali ni wa kutolewa na wao wanaoyakataza. Jee, wanao ushahidi huo? Kama wanao, twaukaribisha.


Hata hivyo, kama ushahidi wanaoutaka wapinga maulidi, wa Qur'ani na Hadithi, ni unaosema kwa kutasua (nassun qat'iyy / categorically), "Enyi mlioamini! Someni maulidi"; basi ushahidi huo hakuna. Lakini tunauliza, kwa sharia ya Kiislamu, ni lazima jambo litasuliwe katika Qur'ani au Hadithi ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) ndipo liruhusiwe kufanywa? Jee, hakuna mambo ambayo Waislamu -- wakiwamo wanaopinga maulidi -- huyafanya pamoja na kuwa hawana ushahidi wa Qur'ani wala Hadithi zilizoyataja mambo hayo?


Kwa mfano, ni nani kati ya wanaopinga maulidi anayeweza kututolea ushahidi wa kutasua -- wa Qur'ani au Hadithi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) -- wa Waislamu kuruhusiwa kujenga vyuo (colleges) na vyuo vikuu? Au kutoa digrii? Au kujenga hospitali na zahanati? Au kujenga nyumba za mayatima (orphanages)? Au kuunda vyama vya ushirika? Au kuweka mashindano ya kusoma Qur'ani na kuyatolea zawadi, na mengine mengi kama hayo? Jibu ni: hakuna! Kama uko, tunaomba tutolewe. Jee, kwa kuwa hauko, ndio watakuwa Waislamu wote -- wakiwamo wanaosoma maulidi -- wanakosea kwa kuyafanya mambo hayo kwa sababu tu hakuna aya au Hadithi inayoyataja? Kama ni hivyo, basi kwa nini wao wanayafanya? Kama sio hivyo, basi kwa nini wanatukataza kuyasoma maulidi kwa sababu hiyo hiyo?Katika Qur'ani na Hadithi kuna mambo ambayo uhalali wake umetasuliwa (specified). Mfano wa hayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kuswali, kufunga (saumu), kutoa zaka, kuhiji, kuowa, kufanya biashara, kufanya uadilifu, na kadhaalika. Kuna na ambayo uharamu wake pia umetasuliwa; kama kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kuzini, kula riba, kuiba, kudhulumu, kusema uwongo, kusengenya, na kadhaalika. Yote hayo ni mambo ambayo ushahidi wake -- wa kuyatasua khaswa -- unaweza kutolewa katika Qur'ani na / au Hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w.).


Kuna na ambayo hayakutasuliwa isipokuwa yametajwa kwa jumla (generally) tu. Hayo, kinyume na yale yaliyotasuliwa tuliyoyataja hapo juu, yana uwanja mkubwa wa jinsi ya kuyatekeleza maadamu hayatachanganywa na ya haramu. Hebu tuangalie mifano miwili mitatu:1. Mayatima: Tunaposoma Qur'ani na / au Hadithi, tunaona kwamba tunahimizwa kwa jumla tuwatizame, tusiwatupe; tuwahurumie, tusiwatese. Vipi? Hilo hatukutajiwa tafsili zake isipokuwa tumeachiwa sisi, bora tu tusitie la haramu. Kwa sababu hii ndio ukaona hakuna aliyezuia kujengwa nyumba za mayatima (orphanages) japokuwa hazikutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)!


2. Ilimu: Tunaposoma Qur'ani na / au Hadithi, tunaona jinsi tunavyohimizwa, bali kufaradhiwa, kusoma na kuitafuta ilimu popote ilipo. Hatukupawa tafsili ya namna ya kulitekeleza hilo. Kwa hivyo, maadamu hatulitii la haramu, tuko huru kusoma kwa ubao, kitabu, tepu, video, redio, runinga, mtandao, na kadhaalika; kama ambavyo tuko huru kusoma madrasa, nyumbani, msikitini, chuoni (college) au kwenye vyuo vikuu; na kama ambavyo tuko huru kukaa majamvini, vitini au madeskini. Hakuna hata mmoja wa mashekhe wa wanaopinga maulidi anayewazuia watu kuyafanya hayo, na tuliyoyataja hapo juu yanayohusu mayatima, kwa sababu tu hayakutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)!


Basi kwa nini kuyapinga maulidi? Inshallah, katika sura inayofuatia, tutazidondoa aya za Qur'ani na Hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambazo, japokuwa hazikutaja maulidi kwa jina, zinaunga kwa jumla yale yanayofanywa na yanayofanyika maulidini.


MAULIDI KATIKA QUR'ANI NA HADITHI Japokuwa -- kama tulivyoeleza katika sura iliyopita -- maulidi hayakutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi, lakini yamekusanya mengi yaliyoamrishwa au yaliyopendekezwa na Qur'ani na / au Hadithi. Hapa chini tutayataja baadhi yake tu:


1. Kusoma na kusikiliza Qur'ani: Tunaposoma Qur'ani (k.m. Sura 73:4 na 20), tunaona jinsi Mwenyezi Mungu anavyotuamrisha tuisome. Na tunapokuja kwenye Hadithi zake, tunaelezwa kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akipenda sana mtu amsomee yeye Qur'ani, na yeye akisikiliza.

Jee, pale tunapoyafungua maulidi yetu kwa mmoja wetu kuisoma Qur'ani, na wengine tukawa tunamsikiliza, huwa -- kama hatukufanya la sunna -- tumefanya lipi la bid'a?


2. Kumswalia Mtume (s.a.w.w.): Katika Qur'ani Tukufu (Sura 33:56), Mwenyezi Mungu anatuamrisha tumswalie Mtume Wake (s.a.w.w.) baada ya kutwambia kuwa Yeye na Malaika Wake hufanya hivyo pia. Isitoshe! Na kila Ijumaa, khatibu hutukumbusha juu ya mimbari, kwa kututajia Hadithi ya Mtume (s.a.w.w.), kuwa yoyote atakayemswalia yeye mara moja, Mwenyezi Mungu atamswalia (atamrehemu) mtu huyo mara kumi!


Jee, katika kikao kimoja tu cha maulidi, waliohudhuria humswalia Mtume (s.a.w.w.) mara ngapi? Zidisha mara hizo kwa kumi ujue Mwenyezi Mungu hukurehemu wewe mara ngapi katika kikao hicho. Jee, ni lipi hapo -- kama halitakuwa sunna -- lililo bid'a?


3. Kumhishimu na kumtukuza Bwana Mtume (s.a.w.w.): Katika Qur'ani Tukufu (Sura 7:157), Mwenyezi Mungu anawasifu, na kuweta "wenye kufaulu", wale ambao humtukuza na kumhishimu Mtume Wake (s.a.w.w.), wakamsaidia na kuyafuata yale aliyoyaleta. Lakini tutawezaje kuyafanya hayo kama mtu mwenyewe hatumjui vilivyo?


Waswahili husema: "Jambo usilolijua ni usiku wa kiza"; na "asiyekujua hakuthamini". Kwa hivyo, bila ya kumjua Mtume (s.a.w.w.) vilivyo -- historia yake, sifa zake, cheo chake, utukufu wake, na kadhaalika -- vipi tutaweza kumthamini na kumtukuza? Ndipo wanazuoni, kwa kuwa si kila mtu aweza kusoma vitabu, wakabuni maulidi ili yawe ni chombo cha kumjulisha Bwana Mtume (s.a.w.w.) apate kuhishimiwa na kutukuzwa. Hivyo katika maulidi, watu hupata fursa ya kuelezwa yote ya Mtume (s.a.w.w.). Na kwa kuyajua hayo, watu humpenda; na kama ilivyo dasturi ya kila apendaye kumfuata yule anayempenda, watu humfuata.


Jee, kama maulidi yanasaidia watu kumjua Mtume (s.a.w.w.), kumkumbuka na kumpenda, ni lipi hapo la bid'a?

4. Kumsifu Bwana Mtume (s.a.w.w.): Tunaposoma maisha yake, tunaambiwa kwamba, miongoni mwa maswahaba, walikuwako waliotunga mashairi ya kumsifu Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambayo walikwenda nayo mbele zake na kumsomea. Bwana Mtume (s.a.w.w.) hakuwafukuza watu hao wala hakuwakataza, bali aliwasikiliza na kuyafurahia yote waliyomsomea. Kwa kitendo hicho kwa hivyo, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alitufungulia mlango wa kumsifu. Tafauti ya pekee iliyoko baina ya maswahaba na sisi ni kwamba wao walimsifu machoni mwake, hali sisi tunamsifu akiwa hayuko na sisi kimwili. Sasa, kwa kitendo hiki, tunafanya jambo gani ambalo halikufanywa na maswahaba na kukubaliwa na mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.w.)?


Kama kufanya hivyo ni bid'a, basi sunna ni ipi?
5. Kutoleana waadhi: Katika Qur'ani Tukufu (Sura 16:125) Mwenyezi Mungu anatuamrisha tulinganiane kwa hikima na mawaidha mema. Na vivyo hivyo ndivyo Bwana Mtume (s.a.w.w.) anavyotuhimiza katika Hadithi zake nyingi. Jee, maulidini hatutoleani mawaidha na kulinganiana mema? Hayo nayo kama ni bid'a, sunna ni ipi?


6. Kumpenda Mtume (s.a.w.w.): Hadithi zake (s.a.w.w.) zatuhimiza tumpende, bali zinatueleza waziwazi kwamba hatuwi ni waumini mpaka tumpende yeye kuliko nafsi zetu, kuliko mali yetu na ahli zetu, bali kuliko watu wote.

Jee sifa zote zile anazosifiwa Mtume (s.a.w.w.) maulidini, furaha zote na nderemo zinazoonyeshwa maulidini, haziwi ni ushahidi wa mapenzi yetu kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.)? Mambo kama hayo hufanyiwa asiyependwa? Kama kuonyesha mapenzi yetu kwa Mtume wetu ni bid'a, sunna ni ipi?


7. Kujumuika na kushikamana: Qur'ani Tukufu (Sura 3:103) inatuhimiza tushikamane na tusifarikiane. Na Mtume naye (s.a.w.w.) anatuhakikishia, katika Hadithi zake, kwamba popote ambapo tutajumuika kwa kheri -- na sidhani kuwa maulidi ni shari -- basi Malaika watatuzunguka, rehema za Mwenyezi Mungu zitufinike, na utulivu wa nyoyo utushukie.


Jee, tunapokusanyika maulidini, hatuyaoni hayo? Ule umoja na mshikamano unaopatikana maulidini, wa wafuasi wa madhihabi mbalimbali kusahau hitilafu zao na kuwa kitu kimoja, ni rehema ndogo?


8. Kutembeleana na kukirimiana: Bwana Mtume (s.a.w.w.), katika Hadithi zake, ametunasihi tuwe tukifanyiana hayo; na hayo huyapata kwa ukubwa siku za maulidi. Waislamu wa mtaa mmoja, au mji mmoja, au hata nchi moja -- kwa kuhudhuria sherehe za maulidi ya wenzi wao -- hupata fursa ya kutembeleana na kukirimiana. Kwa njia hii hujuana hali, wakasaidiana na kupanana (peana) moyo. Hilo huleta mapenzi na mshikamano baina yao. Na iwapo pale pasomwapo maulidi Waislamu ni wachache, kutembelewa kwao na ndugu zao wanaotoka sehemu nyengine huwatia moyo, na pia huwafanya wahishimiwe na wale jirani zao wasio Waislamu. Katika hayo, ni lipi la bid'a, kama hapana la sunna?


9. Kutangaza Uislamu na kusilimisha wengine: Katika Qur'ani Tukufu (Sura 5:67) Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume Wake (s.a.w.w.) awafikishie watu Ujumbe aliompa. Na katika khutba yake ya mwisho, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alituamrisha sisi wafuasi wake tuufikishe Ujumbe huo kwa yule ambaye haujamfikia. Na hilo limepatikana -- na linaendelea kupatikana -- maulidini kwa ushahidi wa rikodi ya wengi waliosilimu baada ya kuhudhuria maulidini na kusikiliza kaswida na khutba zinazotolewa huko.


Jee, bid'a ni ipi hapo?
10. Kumkumbuka Mtume Muhammad (s.a.w.w.): Qur'ani Tukufu (Sura 41:34) inatwambia kuwa jema na ovu si sawa. Ukitaka kuliondoa ovu, liondoe kwa jema ndipo ovu litakapofutika. Na Mtume (s.a.w.w.) naye ametwambia vivyo hivyo. Hali kadhaalika wazee nao wanatwambia kwamba tukitaka kumpokonya mtoto wembe ili asijikate, tusimwache mikono mitupu maana ataurudia. Badali yake tumpe kitu chengine kisicho na madhara (k.m mpira) ashike. Kwa njia hii tutamwokoa na madhara.


Katika zama kama hizi zetu ambapo Waislamu kwa jumla, na watoto wao khaswa, wanayajua zaidi ya viongozi wasio Waislamu, bali hata ya walio maadui wa Uislamu, katika nyanja mbalimbali, na husherehekea mazazi yao -- ni lipi bora? Tuwaache waendelee vivyo hivyo? Au tuwaambie waache kufanya hivyo bila ya kuwawekea badali yake? Au tuwawekee badali iliyo nzuri (ya sherehe za mazazi ya Mtume (s.a.w.w.) na viongozi wengine wa Kiislamu) ili tuwaachishe hayo waliyoyashika? Jawabu hapo ninakuachia wewe, ndugu Mwislamu.

Mpaka hapa tumemaliza majibu yetu ya hujja zinazotolewa na wanaopinga maulidi; na kuwafikiwa ni kwa Mwenyezi Mungu. Sasa, kama tulivyoahidi katika sura ya pili humu, tutayajibu ya Ahlu-Tawheed waliyoyasema katika makaratasi yao, "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulidi". Makala hii imenukiliwa kutoka
http://dir.groups.yahoo.com/group/jifunzeuislamu/message/985?var=1HOJA ZA MAULIDI YA MTUME (S.A.W.W) Ndugu Waisilamu Assalam Alaikum Maulidi ni Kiswahili cha neno la Kiarabu, mawlid. Neno hili lina maana ya "mazazi" au "kuzaliwa kwa

maoni

Acha Maoni

*Mashamba alama ya asteriski ni hakika kuwa thamani.