Kukua fikra za Kiwahabi ni hatari kwa Uislamu

Kukua fikra za Kiwahabi ni hatari kwa Uislamu
Katika hali ambayo viongozi wa Saudi Arabia wanaonyesha msimamo laini na wa upole katika vyombo vya habari kuhusu madhehebu nyingine za Kiislamu, viongozi hao hao wanafanya propaganda kubwa za kueneza fikra za Kiwahabi katika nchi mbalimbali za Kiafrika.

Ripoti ya ABNA-Kituo cha habari cha Jeuneafrique kimeandika makala iliyopewa anwani ya: "Mali, Safari katika Moyo wa Bamako ya Kiwahabi", na kuchunguza maudhui ya hujuma ya Uwahabi katika nchi za Kiafrika na mchango wa wanafunzi waliohitimu masomo katika vyuo vikuu vya Saudi Arabia katika suala hilo.

Mwandishi wa makala hiyo ameashiria suala la kupanuka uhusiano wa kibiashara kati ya Saudia na Mali na kuandika kuwa Uwahabi umeingia nchini Mali kupitia njia ya kustawishwa uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili. Misikiti inayoongozwa na maimam wa Swala za jamaa wenye misimamo ya kupindukia au hata aina ya mavazi ya wanawake yanayoshabihiana na yale ya wanawake wa Kisaudi, yote hayo ni ishara ya kuingia itikadi kali za Kiwahabi katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Mwandishi wa makala hiyo anaendelea kwa kusema kuwa: Mawahabi wa Bamako huamka asubuhi na mapema na kumiminika katika mitaa ya mji huo wakitoa nara na baada ya kushambulia vituo wanavyoamini kuwa vinaeneza misingi ya itikadi zisizokuwa za Kiislamu, hutoweka haraka.

Mwandishi wa makala hiyo anaamini kwamba serikali ya Mali pia imechangia kwa njia moja au nyingine katika kueneza Uwahabi nchini humo. Kwani serikali ya Bamako haijachukua hatua yoyote dhidi ya makundi yanayoeneza Uwahabi nchini humo na wala haiwachukulii hatua za kisheria wale wanaoshambulia raia kwa visingizio mbalimbali. "Kila siku Mawahabi hujenga msikiti katika mitaa na vitongoji vya Bamako, na unapokutana na Wahabi katika misikiti hiyo utamsikia akisema kuwa wao ndio Waislamu halisi na kukulazimisha kufuata itikadi na fikra zao. Huziona amali na ibada za Waislamu wengine kuwa ni makosa matupu na kwamba wao ndio nembo ya Uislamu wa kweli' inasisitiza makala ya mwandishi huyo.

Makala hiyo imeongeza kuwa watu wengi wanaoswali katika misikiti hiyo ni watu waliopata elimu katika vyuo vikuu vya Saudi Arabia. Misikiti mingi kati ya hiyo ina wanafunzi wanaosomeshwa Qur'ani.

Mwandishi wa makala hiyo anamalizia kwa kuandika kuwa wakati kunapofanyika tendo lolote kinyume cha sheria kwa mujibu wa itikadi za Kiwahabi, watu anaoswali katika misikiti ya kundi hilo humiminika mitaani na kushambulia vituo au raia.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa karibu asilimia 90 ya raia wa Mali ni Waislamu.

maoni

Acha Maoni

*Mashamba alama ya asteriski ni hakika kuwa thamani.