Ubora wa Lailatul-Qadr

Ubora wa Lailatul-Qadr

Hivyo basi kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, mwezi mtukufu wa ramadhani ni katika miezi bora mbele ya mwenyezi Mungu kuliko miezi yote, ndivyo hivyo hivyo usiku wa Laylatul Qadri ni bora Zaidi kuliko masiku yote ya mwezi mtukufu wa Ramadha, kama aya zinavyo tuelea na kubainisha sababu kuu za ubora huo, kuwa ni kushuka malaika na kukadiriwa mambo ya waja

Kwajina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu Baada ya kumshukuru Allah muumba na kumtakia Rehema na amani mjumbe wake kipenzi chake mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ali zake waliotoharika na masahaba wake walio wema.
Napenda kuchukua nafasi hii katika jukwaa hili kuzungumzia kwa ufupi ubora na utukufu wa usiku wa Laylatul Qadr na siku zingine, Mwenyezi Mungu mtukufu anasema katika  Qur`an:
 (شهر رمضان الذی انزل فیه القرآن هدا للناس)  
 mwezi wa ramadhani  ambao ndio ambao iliteremshwa ndani yake Qurani iwe ni uongofu kwa watu.
Pia anasema:
إِنَّا أَنْزَلْناهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ وَ ما أَدْراكَ ما لَيْلَةُ الْقَدْرِ لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِنْ أَلْفِ شَهْر(qadr:1-3)
Kwahakika tumeiteremsha Qur`an katika usiku wa Laylatul Qadr. Na kipi kikujulishacho hiyo Laylatul Qadr ?! Laylatul Qadr ni bora kuliko miezi elfu moja.
Mara nyingi zama hutukuzwa na kupewa sharafu kulingana na matukio muhimu yaliyotokea katika nyakati hizo, kiasi kwamba linapotokea tukio baya husifika mwaka huo kwa ubaya wa tukio hilo, kwa mfano mwaka wa Tembo ulifahamika baada ya mfalme Abraha kuvamia mji mtakatifu wa Maka kijeshi ambapo kipando cha Jeshi hilo kilikuwa ni Tembo, hivo ukafahamika mwaka huo kuwa ni mwaka wa tembo, ndivyo hivyo hivyo ilivyokuwa mwaka wa 13 baada ya bwana mtume kupewa Utume ambapo mtukufu Mtume aliondokewa na watu wawili muhimu ambao ni mzee Abu Twalibi na bibi  Khadija (r.a), mwaka ambao mtukufu Mtume(s.a.w.w) aliuita kuwa nimwaka wa Huzuni kutokana na matukio hayo, kwani walikuwa watu muhimu sana kwake.
Mwenyezi Mungu  baada ya kumuumba baba yetu Adamu na Hawaa aliwashusha katika sayari hii ya Dunia na kusema: nendeni katika Ardhi nami nitawatumia uongofu, basi yoyote atakaefuata uongofu huo hatakuwa na hofu wala hato huzunika. Ndipo baadae mola Muumba akaanza kushusha ufunuo kwa Mwanadamu kuanzia kwa Nabii Adamu mpaka Nabii wa mwisho ambae ni mtukufu mtume Muhammad (s.a.w.w), lengo la mwongozo huo ni kumuongoza mwanadamu kweye ukamilifu na uzima wa milele, kwani Mwanadamu bila ya mwongozo  ni sawa na kipando pasina nahodha, na jambo hilo haliyumkiniki kwa mola mwenye Hekima alotakasika na kila upungufu.
Kwa mujibu wa Historia na maelezo ya Dini ya kiislamu ni kwamba; asilimiakubwa ya kanuni na sheria za mwenyezi Mungu katika nyimati zilizopita na uma huu  zilishuka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, na hapa tutaashiria baadhi  ya mambo yanayo ashiria kuwa vitabu vingi vya manabii wakubwa vilishushwa katika mwezi wa Ramadhani.
Imepokelewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) amesema: Taurati imeshushwa mwezi sita, Injili imeshushwa mwezi kuminambili,  Zaburi mwezi kumi na nane na Qur`an  usiku wa Laylatulqadr katika mwezi wa Ramadhani (225 ص4 )مستدرک الوسایل ج.
  Qur`an tukufu ni muongozo wa wanadamu wote wapendao haki na ni kitabu cha mwisho kushuka, kwa maana hakuna kitabu kitakacho shuka baada ya Qur`an tukufu. Moja ya mambo yanayojulisha ubora wa mwezi wa Ramadhani na usiku wa Laylatul Qadr, ni kunasibishwa vitu hivyo kwa Mwenyezi Mungu, na kinachonasibishwa kwa Mwenyezi Mungu bilashaka kinapata utukufu zaidi kutoka kwake, pamoja ya kuwa vitu vyote kwa asili vinarejea na kunasibishwa kwake Mola muumba, lakini mwezi wa Ramadhani na usiku wa Laylatul Qadr kuna tafauti miezi mingine, kwani imepokelewa kutoka katika Hadithi ya mtukufu Mtume (s.a.w.w) kuwa: hakika mwezi wa Ramadhani ni adhimu sana, na mema yatendwayo katika mwezi huo Mungu huyalipa maradufu… hivyo basi ya masiku ya mwezi wa Ramadhani hayafanani na masiku ya miezi mingine.


LAYLATUL QADR   
Mwenyezi Mungu anasema:  "Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu moja". Laylatul Qadri ni miongoni mwa masiku ya mwezi wa Ramadhani ambapo sikuhiyo ni bora kuliko miezi elfu moja, nao ni usiku wa cheo, usiku wa fanaka na neema kwa waja, usiku wa kupitishwa makadirio ya mambo yanayo wahusu waja katika kipindi cha mwaka mzima.
Pia ni usiku wa amani katika ulimwengu na usiku wa kujikurubisha waumini kwa Mola wao na kumuomba maghfira, usiku ambao Shetani hufungwa na kunyimwa uwezo wa kushawishi waja katika maovu mpaka matlai ya alfajiri, ubora ulioje kwa mwenye kukesha na kudiriki usiku huo.
 kwani mwenyezi Mungu ameahidi kwa kila mwenye kumuomba katika nyakati hizo kumkidhia haja zake, ispokuwa kwa watu wafuatao: walevi, wala ngurue, wale wote waliye laaniwa kama wala riba,wala Rushwa, watoa rushwa, wakata udugu, waficha haki, wafitini, wakosa radhi ya wazazi, wazinzi na…) Mungu atuepushe tusiwe miongoni mwa hao) Ama.
kuhusu siku hiyo ,Mtume (s.a.w.w) hakubainisha kuwa ni siku Fulani katika mwezi wa Ramadhani isipokuwa Hadithi za mtukufu Mtume (s.a.w.w) zinaeleza kuwa ni kati ya mwezi 19 au 21 na 23 ambapo Riwaya nyingi zatilia mkazo mwezi 23 ama mwezi 19na 21ni utangulizi na wasila wa kuingia katika usiku huo wacheo ambao ni 23.
Katika usiku huo Mwenyezi Mungu hupanga na kukadiria kila kitu, ndio maana ikaitwa Laylatul Qadri ambapo mema, riziki, Baraka, ajali na umri, majanga na mengineyo ambayo mwenyezi Mungu huyakadiria katika siku hiyo na kuyapitisha, kwa minajili hiyo imepokewa hadithi nyingi sana kutoka kwa watakatifu zinazo wahimiza waumini kukesha katika usiku huo na kumuomba Mola yale yote yalio mema, kwani hiyo ni bajeti ya mwaka na isainiwapo hakuna kupunguza wala kuongeza.
Kwa minajili hiyo kabla hayaja pitishwa mambo yako yamwaka ujao unapaswa kumuomba Mola  wako mambo mema, ama kuhusu mwisho wa fursa hiyo ni mpaka pale inapoingia matlai ya Alfajiri yausiku wa Laylatul Qadr kama ilivyoashiwa katika Qur`an tukufu.
Pia katika Laylatul Qadr mja hulipwa katika kila jema maradufu ya masiku ya kawaida, na Shetani hufungwa katika usiku huo kamavile pia hufungwa milango ya Jahanamu. Kuhusu suala la utukufu na ubora wa Laylatul Qadr na mwezi wa Ramadhani kuna mengi mno yanayoweza kuashiriwa ambapo hatutaweza kuindelea kubainisha zaidi ya hayo tulioyataja kutokana na ufinyu wa Makala hii tumuombe Mola Muumba atuwafikishe sote kuudiriki usiku huu wa Baraka na kushiriki katika mkesha wake.
Hivyo basi kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, mwezi mtukufu wa ramadhani ni katika miezi bora mbele ya mwenyezi Mungu kuliko miezi yote, ndivyo hivyo hivyo usiku wa Laylatul Qadri ni bora Zaidi kuliko masiku yote ya mwezi mtukufu wa Ramadha, kama aya zinavyo tuelea na kubainisha sababu kuu za ubora huo, kuwa ni kushuka malaika na kukadiriwa mambo ya waja
kutoka kwa: Mketo Matenga
mwisho/ 290

maoni

Acha Maoni

*Mashamba alama ya asteriski ni hakika kuwa thamani.